Tuesday, July 05, 2016

HELP FOR UNDERSERVED COMMUNITIES (HUC) KUTOA MSAADA KWA WATU WENYE UALBINO TEMEKE

Na Mwandishi Wetu, Dar

Asasi isiyokuwa ya kiserikali yenye makao yake nchini Marekani, Help for Underserved Communities (HUC), leo itatoa msaada kwa watu wenye ualbino wa wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarfa iliyotolewa na mmoja wa wawakilishi wa asasi hiyo nchini, Nathan Mpangala amesema, HUC itatoa mafuta maalum ya kupakaa, miwani ya jua na kofia kwa baadhi ya wanachama wa Chama cha Watu Wenye Ualbino wilayani humo wapatao 100.
Nathan Mpangala (kulia) akisalimiana na Gaston Mcheka 

Mpangala ambaye pia ni mchora vibonzo maarufu nchini, amesema shughuli hiyo itafanyika katika ofisi za chama hiko zilizopo katika jengo la ofisi za Kata ya Tandika kuanzia saa tano asubuhi, ambapo zinatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa mtaa huo.

Mbali na msaada huo, asasi hiyo pia itatoa ufadhili wa nafasi mbili za masomo ya VETA ngazi ya cheti. “Hii ni nafasi maalum kwa vijana ambao tayari wanafanya shughuli zao mitaani; mfano udereva, ushonaji, kazi za saluni, ufundi umeme, ufundi magari, uselemala nk bila mafunzo yeyote,” amesema Mpangala.

Tangu kuanzishwa kwake, HUC imeshatoa misaada mbalimbali nchini ikiwemo visima, vitabu na ufadhili wa masomo VETA.
Taarifa zaidi kuhusu asasi hiyo tembelea: www.myHUC.org