Friday, May 06, 2016

TAMASHA LA MAJIMAJI SELEBUKA 2016 KUUNGURUMA MEI 28 MPAKA JUNI 4 SONGEA

Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam

KUMEKUCHA, TUKUTANE SONGEA! Lile tamasha kubwa linalosubiriwa kwa hamu na wakaazi wa Ruvuma aka “Bombi hii nyumbi hii” litarindima katika viwanja vya Makumbusho ya Mashujaa wa vita vya Majimaji Mjini Songea, mkoani humo kwa siku nane mfululizo kuanzia tarehe 28 mwezi huu mpaka 4 Juni.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, mratibu wa tamasha hilo Bi. Reinafrida Rwezaura huku akiwa ameambatana na wadau mbalimbali akiwemo balozi wa tamasha hilo ambaye pia ni mchoraji vibonzo maarufu nchini, Nathan Mpangala, amesema tukio hilo linalofanyika kwa mara ya pili, limeandaliwa na Tanzania Mwandi ikishirikiana na Songea Mississippi (SO-MI), ambapo safari hii litapambwa na mbio za ndefu, shindano la baiskeli, ngoma za asili, mdahalo wa wanafunzi wa sekondari, maonyesho ya ujasiliamali/biashara na utalii wa ndani.

Balozi wa Tamasha la Majimaji Selebuka 2016, Nathan Mpangala
Bi. Rwezaura amesema kutakuwa na mbio ndefu za 42km, 21km, 10km (zote za kimashindano) na 5km zisizo za kimashindano maalum kwa wale wanaotaka kupunguza mafuta mwilini. Halikadhali shindano la baiskeli litashirikisha watimua baiskeli toka Rwanda na nchi nyingine za jirani.

Kutokana na upekee wa tamasha hili, litatoa fursa kwa wajasiliamali toka Ruvuma na mikoa mingine kuibua na kutambua fursa za kiuchumi zilizopo mkoani humo hivyo umetolewa wito wajitokeze kwa wingi ili kupanua masoko yao.

Imeelezwa kuwa tamasha hilo linalenga pia kukuza elimu kupitia mdahalo wa shule za sekondari na kuibua fursa za kitalii zilizopo mkoani humo kupitia utalii wa ndani.  

Bi. Rwezaura amesema tamasha litazinduliwa kwa mbio ndefu tarehe 28 Mei 2016, saa 12 asubuhi na kufungwa na shindano la baiskeli siku ya kilele, tarehe 4 Mei, ambapo ulinzi na usalama utakuwepo wa kutosha

Bi. Reinafrida Rwezaura

Amesema zawadi mbalimbali zitatolewa ikiwemo vikombe, ngao, vyeti, fedha taslimu na zawadi nyingine nyingi.  Mbali na zawadi hizo, washindi watatu wa baiskeli watapelekwa Rwanda kwenye mafunzo ya mbio za baiskeli za kimataifa.

Bi. Rwezaura amesema viwango vya ada ya ushiriki ni kama ifuatavyo;
Mbio ndefu 42km – 10,000/=, 21km – 5,000/=, 10km – 3,000/= na 5km – kundi hili ni mbio za kujifurahisha, hakuna kiingilio.
Atakaependa kushiriki shindano la baiskeli za 50km atachangia – 10,000/=, ngoma za asili  kila kikundi – 10,000/=, maonyesho ya ujasiliamali kikundi – 50,000/= na mtu mmoja mmoja – 10,000/=

Kwa maelezo zaidi na fomu za ushiriki zinapatikana kupitia:  www.somi.international au www.tanzaniamwandi.com

Wakati huo huo, mchoraji vibonzo maarufu nchini, Nathan Mpangala aka Kijasti ameteuliwa kuwa balozi wa tamasha hilo.

Akizungumza baada ya uteuzi amesema, anashukuru kupewa heshima hiyo ya kipekee na ametoa wito kwa watu mbali mbali kujitokeza kwa wingi Songea kwani ni tamasha la kipekee litakalokuwa na fursa nyingi.

“Wajibu wangu ni kuhamasisha na kwenda kushiriki. Nitafanya onesho la vibonzo na jinsi ninavyovichora kuanzia hatua ya kwanza mpaka mwisho, halikadhalika nitashiriki katika mdahalo wa wanafunzi, utalii wa ndani na riadha,” amesema Mpangala.

Nguli huyo wa vibonzo amedai kwa sasa anajifua mara tatu kwa siku ili kujiweka fiti tayari kuwagalagaza washindani wake katika riadha.