Wednesday, April 06, 2016

JE, UNAPENDA KURASIMISHA KAZI YAKO YA SANAA? TARATIBU HIZI HAPA...

BARAZA LA SANAA LA TAIFA (BASATA)
TARATIBU ZA KUPATA USAJILI NA KUTAMBULIWA

Utangulizi

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ni Shirika la umma lililoundwa kwa Sheria ya Bunge Na. 23 ya Mwaka 1984. Pamoja na kazi nyingine za Baraza zilizoanishwa katika Sheria hii, Baraza lina jukumu la kusajili na kutoa vibali kwa wale wote wanaojishughulisha na shughuli za Sanaa na Burudani Tanzania Bara. (“Ni kinyume cha Sheria kujishughulisha na shughuli za Sanaa na burudani bila ya kibali cha BASATA”). Aidha, Baraza lina mamlaka ya kufuta usajili, kusimamisha shughuli, kusitisha kwa muda au kutoa adhabu nyingine kwa yoyote anaekaidi Sheria hii.

Wanaotakiwa kusajiliwa na Baraza ni:

·       Wasanii binafsi (ikiwa ni pamoja na walio katika vikundi mbalimbali)
·       Vikundi vya wasanii
·       Vyama
·       Mitandao ya wasanii
·       Mashirikisho ya Wasanii
·       Taasisi
·       Kampuni
·       Studio za kurekodi muziki na
·       Kumbi za Sherehe na Burudani

Utaratibu wa kujisajili
a) Chukua fomu ya maombi ya usajili kwa Afisa Utamaduni wa Wilaya ulipo, Ofisi za BASATA, au katika tovuti ya Baraza (http://www.basata.go.tz/downloads.php ).   
Jaza fomu nakala 3 na uambatanishe na
·         Katiba nakala 3 (msanii binafsi aambatanishe wasifu wake si katiba)
·         Picha(passport size) nakala 3 za kila kiongozi wa kikundi/taasisi/kampuni n.k.
·         Nakala ya muhtasari wa kikao cha wanachama/wamiliki wa kujadili kusudio la kujisajili      na kuipitisha Katiba, pamoja na majina ya waliohudhuria na sahihi zao.
·         Nakala ya hati ya mlipa kodi (TIN)
b)  Pitisha maombi yako kwa Afisa Mtendaji wa Mtaa/Kijiji aidhinishe.
c)  Pitisha maombi yako kwa Afisa Utamaduni wa Wilaya aidhinishe.
d)  Wasilisha maombi yako BASATA.

Faida za kujisajili na kufanya kazi kwa kushirikiana na BASATA
·   Kuendesha shughuli kwa mujibu wa sheria za nchi.
·  Kuwa rasmi/kutambuliwa kwa shughuli ya msanii binafsi, kikundi, chama n.k hivyo kufanya kazi kihalali
·   Kupata ushauri wa kitaalamu kuhusiana na kazi za Sanaa
·  BASATA kama shahidi wa Jamhuri hutoa utambulisho wa msajiliwa mahali popote panapohitajika kwa mfano wakati wa kufungua akaunti, shahidi mahakamani n.k.
·   Kusaidia pale kazi itakapohitajika kuwekewa ulinzi kisheria, kwa mfano kumtambulisha msanii COSOTA ili kuthibitisha kama kazi imefanywa na msanii/ kikundi au chama kinachotambulika kisheria.
·   Kuwa karibu na wasanii na wadau wa sanaa kwa kutafuta na kusambaza taarifa za fursa zinazopatikana katika tasnia ya sanaa mfano: maonesho na matamasha ya nje ya nchi.
·    Kusaidia kutatua masuala yahusuyo haki za wasanii zinaporipotiwa na wasanii.

Ada ya kibali kwa mwaka (kuhuishwa kila mwaka)
·       Msanii binafsi Tsh 40,000
·       Kikundi Tsh 40,000
·       Chama Tsh 50,000
·       Mtandao Tsh 50,000
·       Taasisi Tsh 50,000
·       Kampuni Tsh 200,000
·       Studio Tsh 200,000
·       Kumbi 300,000 – 1,000,000 (kulingana na hadhi na sifa ya ukumbi)

Gharama za usajili: Makundi yote yatalipia ada ya usajili Tsh 30,000 na gharama ya fomu Tsh 5,000 (gharama hizi hulipwa mara moja tu)

NB: Kwa walioko mikoani unaweza kutuma maombi yako kupitia kwa Afisa Utamaduni wa Wilaya, kufika BASATA au kutuma moja kwa moja BASATA kwa njia ya Posta. Kwa maoni na maelezo zaidi wasiliana nasi kupitia:

Katibu Mtendaji,
S.L.P 4779, Dar es Salaam- Tanzania
Ilala Sharif Shamba,
Simu : Tel: 2863748/2860485
Faksi : 0255 - (022) - 286 0486

Barua pepe : basata06@yahoo.com