Monday, March 07, 2016

WANAFUNZI WA KIKE HUKOSA MASOMO KATI YA SIKU 3-5 KILA MWEZI! SABABU HII HAPA…

Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WANAFUNZI wa kike wenye afya nzuri wana nafasi nzuri ya kushiriki masomo kikamilifu, kufaulu na hatimae kutimiza ndoto zao kwa kushiriki shughuli za ujenzi wa Taifa.

Akizungumza na kurasa huu, leo, Bi. Joyce Thomas toka kituo cha Tafiti za Afya na Maendeleo - TAI cha jijini Dar es Salaam, amesema moja ya mambo yatakayosaidia kufikiwa kwa usawa wa kijinsia ni pamoja na kuhakikisha wanafunzi wa kike wanapatiwa elimu ya afya kuhusu miili yao.

Bi. Joyce Thomas kutoka Kituo cha Tafiti za Afya na Maendeleo, akitoa mafunzo kwa baadhi ya wanafunzi wa kike wa Jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
“Tafiti zinaonyesha wanafunzi wa kike hukosa masomo kati ya siku 3 hadi 5 kila mwezi kutokana na ukosefu wa uangalizi kipindi cha hedhi. Maumivu ya tumbo na kukosa kujiamini huwapotezea mwelekeo hivyo kushindwa kufanya vizuri kwenye masomo,” amesema Bi. Joyce.

Bi. Joyce ametoa rai kwa wanafunzi wa kike pindi waingiapo katika hali hiyo, waepuke kutumia kahawa, wajiamini, waipokee kwani ni suala la kibaolojia na wafanye mazoezi ili kupunguza maumivu.

Pia, amewashauri wazazi na walezi kutumia maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Duniani, kesho, pamoja na mambo mengine, wazungumze na wanafunzi hao kuhusu suala hilo kwani kwa kufanya hivyo watawawezesha kuijua miili yao hivyo kushiriki masomo bila wasiwasi.