Tuesday, March 08, 2016

WACHORA VIBONZO WAASWA KUJITOKEZA KUGOMBEA NAFASI ZA UONGOZI SHIRIKISHO LA SANAA ZA UFUNDI. UCHAGUZI KUFANYIKA MWEZI HUU

Nathan Mpangala, Dar es Salaam

SHIRIKISHO la Sanaa za Ufundi Tanzania – TAFCA litafanya uchaguzi mkuu tarehe 31 mwezi huu.

Kwa mujibu wa taarifa fupi iliyotolewa na Katibu Mkuu wa shirikisho hilo Bw. Godfrey Ndimbo inasema, nafasi zitakazogombewa ni Urais, Umakamu wa rais na ujumbe.

Fomu za wagombea zimetolewa jana Jumatatu ambapo ya Urais inapatikana kwa kwa Tshs 80,000/-, Makamu rais Tshs 60,000/- na Ujumbe Tshs 50,000/-.

Taarifa hiyo imesema maelezo zaidi yanapatikana kwa Katibu Mkuu huyo kupitia nambari 074 283 380.

Wakati huo huo, mjumbe wa Chama cha Wachoraji Vibonzo Tanzania, Bw. Fadhili Mohamed amewataka wachora vibonzo nchini kujitokeza na kushiriki kikamilifu mchakato huo ili kupata viongozi bora watakaotetea haki zao na kusimamia maendeleo ya wasanii wa sanaa za ufundi kwa ujumla.

Bw. Fadhili Mohamed

“Umefika wakati sasa mambo haya ya kuchagua viongozi tusifanye kama ya fulani na fulani na wewe kujiona umebanwa na shughuli. Tukipuuzia hili suala kesho tusijekulalamika endapo uendeshaji wa shirikisho utakuwa dhaifu maana maamuzi yote tunatakiwa kufanya sasa kama wahusika na si kusubiri kuchaguliwa na wenzetu,” amesema Mohamed.


Mjumbe huo ambaye ni maarufu kwa kibonzo cha Kabwela amesema, wachoraji vibonzo wana changamoto nyingi ambazo zimekuwa zikirudisha nyuma maendeleo ya wachora vibonzo na wasanii wa sanaa za ufundi kwa ujumla. Ili kukabiliana na changamoto hizo lazima tupate viongozi wa shirikisho wenye uwezo, uvumilivu na kujitoa kwa ajili ya wengine, nao hao watatoka miongoni mwetu sisi.

  
Wasanii ambao wanahaki ya kugombea uongozi katika shirikisho la sanaa za ufundi ni pamoja na wachoraji wa rangi, wachora vielelezo, wachora vibonzo, wachoraji wa kwenye vyuma na mbao, waandishi wa herufi, watengeneza animeshini, wachora ramani, wafinyanzi, wachongaji, wapigaji picha za mgando,  wasanifu majengo, wasanii wa viwandani, waendesha ulimbwende, wasusi na wabunifu wa mavazi.