Saturday, March 05, 2016

ULAYA HAKUNA UBWETE, UKITAKA KWENDA ‘KUSHANGAA’ UWANJA WA TIMU YA SAMATTA JIPANGE

Nathan Mpangala, Dar es Salaam

MASHABIKI, watalii, vikundi na watu mbalimbali leo watapata nafasi ya kutembelea uwanja wa Klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji ikiwa ni utaratibu iliyojiwekea ambapo kila Jumamosi ya kwanza ya mwezi hukaribisha wageni kwenda ‘kushangaashangaa’ kiota chao maarufu kwa jina la Cristal Arena. Sio bure, kwa malipo.

'Shamba' la Genk, Cristal Arena
'Washangaaji' wataanzia mahala panapoitwa Goal Mine; kitovu cha taarifa za Genk. Kisha watapitishwa sehemu kadhaa; kama vyumba vya kubadilishia nguo, chumba cha habari, sehemu ya wageni, viwanja vya kukuzia vipaji, mahala pa kumbukumbu, duka la klabu na 'kona' nyinginezo.

Kwa mujibu wa taarifa toka mtandao wa Genk inasema, tukio hilo litaanza saa 7.30 mchana huu na kumalizika saa 10.30 alasiri, ambapo ‘watu wa karibu’ wa Genk watalipia kiasi kinachokadiriwa kuwa 22,500/-, walivuka miaka 55 na watoto chini ya miaka 6 wao watalipia kama 17,500/-.

Kwa wasio ‘marafiki’ wa Genk, wao watakamuliwa 'araundi' 27,500/- hivi, ‘wazee’ na watoto chini ya miaka sita watalipia 22,500/-.

Swali, hili limekaaje kwa timu zetu za hapa nyumbani, hasa hao wanaotamba kuwa ndio wenye mpira wao Bongo, Simba na Yanga? (Picha: Tovuti ya Genk)