Thursday, March 03, 2016

SIJIPI STRESI. NGULI THIERRY HENRY ALISHASEMA, WENGER NUNUA STRAIKA, ARSENAL HAIWEZI KUSHIDA UBINGWA KWA KUMTEGEMEA OLIVIER GIROUD


Nathan Mpangala, Dar es Salaam

IKICHEZA nyumbani, huku ikijua fika kuwa juu kuna dogo mtukutu, Leicester mwenye pointi 57 anasumbua, Arsenal imekubali kichapo cha goli 2-1 toka kwa Swansea iliyo katika nafasi 16 katika mechi ya Premier League iliyopigwa Emirates, jana. Arsenal bado imekwama katika nafasi ya tatu na pointi zake 51.

Matokeo hayo, yamenifanya niukumbuke ushauri wa aliyekuwa mshambuliaji mwiba wa Arsenal, aliyewageuzageuza wapinzani atakavyo pale mitaa ya Highbury (sasa Emirates), Thierry Henry (kushoto), aliyemshauri Wenger kununua wachezaji wanne wa kiwango cha juu kama kweli ana nia ya kubeba kombe la Premier League tena.

Thierry Henry aliyasema hayo mwezi April mwaka jana, kwamba klabu yake hiyo ya zamani, ina tatizo kubwa kubwa kwenye mhimili wa timu, hivyo ilishauri ivute vichwa vinne vya kiwango cha juu duniani, vinginevyo ikiendelea kumtegemea Olivier Giroud (chini kulia) kama straika namba moja, habari ya ubingwa isahau.

Mfaransa huyo aliishauri Arsenal izame mfukoni, isajili wachezaji wenye viwango vya juu kabisa ili wasaidie kufukuzia ubingwa ambao wanausaka toka walipoubeba kwa mara ya mwisho 2004.

Henry alisema: "Nadhani wanahitaji kununua wachezaji wanne – ili kuimarisha mhimili wa timu. Wanahitaji golikipa (akanunuliwa Petr Cech), beki wa kati, kiungo mkabaji na mshambuliaji wa kiwango cha juu.

"Sikatai Giroud ni mchezaji mzuri. Lakini najiuliza unaweza kushinda ubingwa kwa kumtegemea? Sidhani.” Alisema Thierry Henry.

Wenger shaurika basi kidogo babu yanguuu, mashabiki huku Bongo (mimi simo kabisa) wanaumia mioyo, kha! (Chanzo: http://www.mirror.co.uk)