Friday, March 04, 2016

PAMOJA NA KUWA KUKU NI KUKU TU LAKINI YAPO YA KUJIFUNZA TOKA KWAKE HASA JIKE

1. Pamoja na kuwa hajashiriki kozi hata moja lakini anajua kujipanga. Kwanza hutaga mayai, kisha huyalalia: MPANGO MAKINI.
2. Dah, kuku yuko makini jamani! Akishaanza kulalia, hupunguza nyendo. Muda mwingi hutulia kiotani: CHEKI NIDHAMU HIYO.
Kuku katika majukumu yake ya kawaida
3. Wakati wa kulalia hupungua uzito kutokana na kutukupata menyu kwa wakati: HIYO INAITWA KUJITOA MHANGA.
4. Masikini, kuku hanaga hiyana, anaweza kulalia hata mayai yasiyo yake: MAMBO YA UBAGUZI HANAGA.
5. Hulalia kwa siku 21, hata pale mayai yanapochelewa ‘kuiva’ huokomaa tu mpaka kieleweke:  AMEJAWA NA IMANI, MATUMAINI NA HUJIPA MOYO.
6. Anapogundua mayai yaliyoharibika, kiroho safi huyasogeza pembeni ili asiendelee kuyalalia: DAH, CHEKI ALIVYO NA UFAHAMU.
7. Huachana na mayai vinza na kuanza kulea vifaranga hata kama ni kimoja: ANAKUBALI UHALISIA.
8. Hataki kabisa kuona vifaranga vyake vinachezeshwa ngololo na mtu au kiumbe yeyote: HUO UNAITWA ULINZI TOKA MOYONI.
9. Mara zote huwa hachezi mbali na vifaranga: UKISIKIA UMOJA NDIO HUO.
10. Hulea vifaranga vyake mpaka pale vinapokua na kuanza kujitegemea: HURITHISHA MBINU ZA KUJITEGEMEA.