Thursday, March 10, 2016

MWANDISHI SALEH ALLY ASHANGAZWA NA UPANDE WA PILI WA SHILINGI WA NIGERIA

Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MWANDISHI NGULI wa habari za michezo nchini, Saleh Ally, hivi karibuni alikanyaga jiji la Lagos, Nigeria kwa minaajili ya kuhudhuria Tuzo za Filamu maarufu African Magic Viewers Choice Awards (MVCA), ambazo Watanzania wawili; Single Mtambalike "Rich Richie" na Elizabeth Michael "Lulu" waliibuka kidedea.

Macho hayana pazia, ukiacha hilo lililompeleka, yapo mengine meeeengi aliyoyaona. Kula ushuhuda huu…

“Ninachotaka kuzungumzia hasa ni kile nilichojifunza baada ya kufika Lagos. Kwa kuwa nimesafiri katika nchi nyingi za Afrika, nilijua Lagos utakuwa ni mji wa aina yake hasa kutokana na kelele nyingi za Wanigeria kuusifia au kuisifia nchi yao,” anasema Saleh.


“Nafurahi wenyeji wangu walinichagulia hoteli nzuri kabisa ambayo sikuwa na shida zaidi ya kufurahia maisha. Lakini tokeo nilipofika, kila kitu ilikuwa ni kushangaa tu kwangu na si kwa ubora au uzuri wa mambo, badala yake hali mbaya ambayo sikutegemea kuiona,” anazidi kushuka Saleh.

Saleh anasema Tamasha la tuzo lilifanyika kwenye kisiwa kidogo cha Victoria, hiki ndiyo kinaonekana kuwa na mvuto lakini bado kwake hakukuwa na cha ajabu kwa maana ya ubora. Kuanzia Victoria hadi Lagos, bado hakukuwa na ubora wa kumshangaza. Maana kila kitu kinachoweza kuwa bora, alishakiona nyumbani na vingi vya Tanzania ni bora zaidi.

Mwenye macho haambiwi...

Anaendelea kusema wana maghorofa marefu, lakini ubora wa ujengaji na mvuto hakuna kitu. Uwanja wa Ndege wa Muhammed Murtara ni mkubwa kuliko wa Julius Nyerere wa Dar es Salaam. Lakini kimfumo, utendaji wa kazi ni hovyo, hakuna lolote.


Akizungumzia makazi Saleh anasema, makazi ya watu karibu na katikati ya jiji ni hovyo kabisa, machafu, si salama kwa afya na yenye hali ya kushangaza kabisa. Hakika sikutegemea kuyaona hayo Nigeria maana niliamini ni nchi iliyoendelea sana na kamwe hatuwezi kuisogelea kwa kuwa wameanza mapambano ya maendeleo kitambo.

Suala la nidhamu nalo shida. “Niligundua maisha ya Nigeria wengi hayana nidhamu katika mambo mengi; msongamano ni mkubwa, barabara za lami lakini mbovu, milango ya daladala inafungwa kwa kamba au mipira! Hakika nilishangaa kuzidi kipimo” anasema Saheh.

“Sijalenga kuwaudhi Wanigeria au kuwadhihaki, lakini nimejifunza kwamba nastahili kufanya hivi; Kwanza kuongeza mapenzi kwa nchi yangu Tanzania, nitaendelea kuipigania kila siku, kila nitakapoweza. Pili, kuendelea kuitangaza kwa nguvu kwa kuwa Wanigeria wanajua kwao kiutaratibu na maisha yalivyo ni sehemu ya kawaida tu. Lakini sifa na matangazo yao kwa dunia nzima wanataka paonekane ni moja ya sehemu bora za Afrika lakini kumbe hakuna lolote.’ Anasema Saleh.

Saleh anamaliza kwa kusema, ipende Tanzania yako kwa kuwa ndiyo sehemu bora kabisa ya kuishi kuliko nyingine zote Afrika, ikiwezekana kuliko zote duniani kote. NAKUPENDA TANZANIA.

Ukurasa huu, unakupongeza Saleh Ally kwa kushirikisha Watanzania kwenye jambo hili ambalo husaidia kujipima kama Taifa.