Friday, March 11, 2016

MCHORA VIBONZO MAARUFU KULIBURUZA GAZETI LA NATION MAHAKAMANI

Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

KIMENUKA! Mchora vibonzo maarufu Godfrey Mwapembwa maarufu Gado, anajipanga kulishtaki gazeti la The daily Nation la nchini Kenya kuhusu kile alichokitaja kuwa kusimamishwa kazi kinyume cha sheria.

Mchoraji huyo wa Kitanzania ambaye amekuwa akiishi na kufanya kazi Kenya kwa miaka mingi, ameiambia BBC kuwa mwaka jana alichukua likizo kufuatia kile alichosema ni kuingiliwa kwa kazi yake.

Godfrey Mwampembwa aka Gado
Gado amesema kwamba aliwahi kuchora kibonzo katika gazeti jingine kuhusu aliyekuwa rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete ambacho anasema hakikumuangazia vizuri.

Inadaiwa mhariri wake wa gazeti hilo alipendekeza kwamba apumzike kwa kuwa sio mfanyakazi kamili wa gazeti hilo wakati huohuo tayari alikuwa na mkataba nao mpaka Julai mwaka huu.

Hata hivyo, mwezi uliopita alipewa barua ya “kunawishwa kibarua” huku gazeti hilo likisisitiza kwamba, kuachana uliafikiwa na pande zote mbili.

Lakini mchoraji huyo anaamini kwamba “kutimuliwa” kwake kunatokana na shinikizo la kisiasa akiongezea kuwa anaamini kwamba serikali ya Uhuru Kenyatta imekuwa haipendezwi na kazi yake.

Gado ni mchora vibonzo maarufu nchini Kenya ambaye huwachekesha wasomaji wengi kwa uchoroji wake.

Mtandao wake unaomtaja kuwa mchoraji vibonzo hodari wa kisiasa katika eneo la mashariki na Afrika ya kati. Gado anasema kuwa vibonzo vyake huangazia masuala mbalimbali, yakiwemo ya ugaidi, ukataji miti, ukimwi na ufisadi na vibonzo vyake vimekuwa vikizua mjadala mkubwa. (Chanzo: http://www.bbc.com/swahili)