Wednesday, March 09, 2016

DUNIA YA 50-50 IFIKAPO 2030: ONGEZA JUHUDI KULETA USAWA WA KIJINSIA – INA MANTIKI

Chiku Lweno-Aboud, Dar es Salaam

Machi 8 ni Siku ya Wanawake Duniani. Kama mwanamke najua yanayosibu. Kama mwanaharakati nazifahamu propaganda. Kama binadamu, nauliza KWA NINI!!!
Kauli mbiu ya Siku ya Wanawake Duniani 2016 ni Dunia ya 50-50 ifikapo 2030: Ongeza Juhudi kuleta Usawa wa Kijinsia – Ina Mantiki

Wala hatutakiwi kulidai hili. Kwani ni jambo lililo wazi kabisa. Uwiano wa watu duniani kwa misingi ya jinsia ni  50-50… Lakini ni kwa nini tunahitaji kudai jambo hili?

Kwa nini?
Nauliza kwa nini mateso hayaishi? Uonevu na unyanyasaji pia haukomi…? Hivi kukomesha haya ni wajibu wa nani hasa. Katika moja ya safari zangu za kampeni, nilifika kwenye kijiji kimoja cha Wamaasai na niliongea na makundi mbali mbali juu ya athari ya ukeketaji.


Basi ikawa muda wa kuongea na wazee wa Kimaasai.... na kabla hatujaanza mjadala waliniuliza kwa upole tu, ni kwa nini naongea na wao kuhusu ukeketaji wakati ninafahamu kuwa ni "wanawe ndio wanaowafanyia wanawake wenzao na wasichana huo ukeketaji" na hivyo jambo hilo haliwahusu wanaume. Kweli?

Kwa hiyo nikawauliza, sio ninyi mnaotoa ruhusa, muongozo na baraka za ukeketaji kwenye jamii kwa kuwa hamkubali kuoa wanawake ambao hawajakeketwa? Sio ninyi mnaotoa maamuzi wakati muafaka binti zenu kukeketwa kwa sababu wakipitia mila hiyo wataolewa nanyi mtapata ng'ombe wengi? Hivi mnafahamu kuwa kuna wanawake nchi hii hii ambao ni wa makabila mengine  na hawakeketwi lakini  wanaishi maisha mazuri tu--na pia huolewa?

Ni kwa nini watu wanataka kuamini kuwa ukatili, uonevu na unyanyasaji unaompata msichana au mwanamke hauwahusu wao? Huchukua njia ya mkato na kujisahaulisha kuwa yule angeweza kuwa ni binti yao, mama, dada, bibi au kwa lugha rahisi sana, ni binadmu!Haya na tusogeze siku mbele hadi wiki hii. Ninanakili hapa ujumbe ambao kwa mara ya kwanza mwandishi aliuweka kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook...

Acha mara moja!
 “Machi 8 ni Siku ya Kimataifa ya Wanawake na nilitaka kuwashirikisha nanyi kuhusiana na tukio lililotokea usiku wa Jumamosi. Nilikuwa nimeegesha gari langu kwenye Tamasha la Nyama Choma Festival na nyuma ya gari iliyokuwa karibu alikuwemo mwanamke aliyekuwa akishikiliwa kwa nguvu na mwanaume, bila ridhaa yake. Ilikuwa kama amemkumbatia na kumzuia kwa nguvu huku yule binti akihangaika na kulia kuomba aachiwe.
Kulikuwa na wanaume wapatao 7 (miongoni mwao walinzi 2) waliokua ndani ya eneo la kama mita 5 hivi kutoka eneo la tukio. Niliwaomba baadhi yao kuingilia kati na hawakufanya lolote, badala yake walinipuuza au kusema tukio lile lilikuwa haliwahusu.

Mwishowe nikaenda mwenyewe, nikaweka mkono wangu kwenye mkono wa yule mwanaume aliyekuwa akifanya ukatili, nilimuangalia moja kwa moja machoni na kwa mkazo nikamuambia amuache yule mwanamke.
Ilinibidu kurudia kauli yangu kama mara sita hivi lakini nilifanikiwa - akalegeza mikono na yule binti akakimbia (huku akinishukuru kwa dhati kabisa).

Sasa hivi najua kulikuwa na yaliyojiri kabla ya pale lakini sijali: Hakuna mwanaume yoyote mwenye haki ya kumshikilia na kumzuia kwa nguvu, au hata kumgusa mwanamke bila ridhaa yake. Marafiki, tafadhalini tuyachukulie matukio ya hivi kwa uzito na kuona yanatuhusu, pale ukatili wa kijinsia unapojitokeza.


Asante na heri ya Siku ya Wanawake kwenu wote... Beth Jere." Alimalizia hivyo.
Kwa kweli niliishiwa maneno. Nilichoandika kujibu pale chini ni maneno achache tu. "Mungu akubariki!."

Ujumbe ule ulisombwa na kusambazwa na watumiaji wengi wa Facebook hasa wakazi wa Dar es Salaam. Unajiuliza ni kwa nini watu wana uvumilivu na ukatili kwa binadamu mwingine, hasa akiwa ni mwanamke ?

Tunahitaji kuongeza juhudi zaidi
Naandika makala hii kama wajibu wangu. Kama mwanaharakati, kama mwanamke na kama binadamu. Lakini nisingeweza kuacha fursa hii ya kuandika ipite kwa sababu ni mwanaume aliniomba niandike makala/blogu ili aweke kwenye tovuti yake mahsusi kwa ajili ya Siku ya Wanawake Duniani. Nathan Mpangala, Mungu akubariki nawe pia na tafadhali endelea na utetezi wa haki kwa binadamu wote.

Tunahitaji watu wengi zaidi wazungumze kwa uwazi kuhusu haki na usalama wa mwanamke, waonyeshe msimamo na la muhimu zaidi, WACHUKUE HATUA dhidi ya uonevu na uvunjaji wowote wa haki za wanawake.

Wanawake ni nusu ya idadi ya watu wote ulimwenguni, hivyo basi kauli mbiu ya Dunia yenye uwiano sawa wa 50-50 by 2030: Ongeza juhudi kuleta Usawa wa Kijinsia ina mantiki. Beth, Nathan, na wengine wote… Heri ya Siku ya Wanawake Duniani! 
(Chanzo: http://www.mamaye.or.tz/, Michoro: Nathan Mpangala)