Friday, February 26, 2016

UNATAKA KUWA MCHORA VIBONZO? SIRI HII HAPA

MCHORA vibonzo maarufu nchini, Nathan Mpangala (pichani) anawashauri nini vijana wenye ndoto ya kuja kuwa wachora vibonzo mahiri? 

Kwanza jiulize, unataka kuwa mchora vibonzo vya aina gani? Kisiasa? Kiuchumi? Kijamii? Michezo? Stripu? Au hadithi za michoro? Unataka kuchorea magazeti au mitandao? Au unataka ‘upige’ kotekote? 

Mbili, kipi kinakusukuma kutaka kugeuza kitu unachokipenda tu moyoni yaani kuchora kuwa kazi? Ni swali la mzaha lakini zito. Upande wa pili wa swali uko hivi, tufanye unapenda sana kula vitumbua, je, unaweza kugeuza kupenda huko kuwa kazi rasmi ya kukuingizia kipato? Usicheke, tafakari.Mchora vibonzo mtarajiwa, sasa kamata mistari ambayo nina hakika hutapenda kuisikia. Fani ya uchoraji vibonzo haina malipo mazuri. Ukijitosa suala la ‘fuba’ sahau. Huko ni fulu wito. Ni kazi inayokula muda. Mazingira ya vyombo vingi vya habari si rafiki kiviiiile. 

Wanunuzi wa magazeti ni wa kubipu. Nafasi za kuchora magazetini ni finyu. Wakati mwingine inabidi ukae kwenye foleni mpaka mtu asuse, atimuliwe, ahame, astaafu au arudishe namba ndipo uzibe nafasi yake! Utaanza na kuchora katuni moja kwa wiki ambayo malipo yake ni kama buku tano! Sikukatishi tama, ukikomaa utakomaa utavuka.

Uwepo wa mashindano ya kumwaga ya vibonzo yasiyo na zawadi zilizoshiba (hasa huko duniani), malipo madogo, uhaba wa magazeti ya kuchorea hufanya wachora vibonzo kujawa stresi hali inayosababisha vibonzo kukosa ucheshi badala yake huwa vituko. Wapo wachora vibonzo wakubwa duniani wanaishi maisha ya kifukara, wana mastresi ya kumwaga na wanajuta kwa nini hawakuchagua kazi nyingine.


Bado una nia? Safi, kula huu ushauri:
1. Fanya mazoezi ya kuchora sana ili ukuze kipaji chako. Ninaposema sana iwe sana. Lengo lisiwe kuwa mchoraji mkubwa bali uwe na maono ya kuchora kwa kiwango bora kupita waliokutangulia ili kuinua taaluma ya uchoraji kwa ujumla.

2. Jichanganye, tandaa, kongamana, shiriki mikutano na mafunzo mbalimbali. Hakikisha watu wanaona kazi zako.
3. Kuwa mbunifu. Chora vitu mbali mbali hata usivyovipenda.
4. Unapokuwa kwenye mijadala,  iwe mitandaoni au laivu tupia pointi zenye mashiko.
5. Sambaza vibonzo vyako kwenye magazeti mbalimbali, tovuti, na tv. Wakati wote hakikisha unajisogeza kwa watu wanaofanya kazi katika vyombo vya habari.
6. Hakikisha unapata machapisho yenye vibonzo na taarifa za wachoraji.
7. Jitambulishe kwa taasisi mbalimbali kuwa wewe ni mchora vielelezo za vitabu, mabango, vipeperushi nk.
8.Jifunze jinsi ya kujiendesha kibiashara. Mfano, tafiti viwango vya malipo ya vibonzo na jinsi ya kupanga bei.
9. Kama kuna kazi nyingine pembeni unafanya, usiiache.
10. Ukishatia nia, usikate tamaa. Komaa utatoka.