Monday, February 29, 2016

SAMATTA AANZA AMSHAAMSHA ZAKE GENK, AICHEZESHA NGOLOLO CLUB BRUGGE

IKICHEZA uwanja cha nyumbani Cristal Arena, mbele ya mashabiki waliopagawa, Mbwana Ally Samatta, jana, ameithibitishia KRC Genk ya Ubelgiji kwamba haikukosea kumvuta kundini baada ya kucheka na nyavu ya manunda Club Brugge na kuifanya timu yake kuibuka na ushindi wa bao 3-2.

Mpika bao ( Malinovskyi) akimpongeza mpiga bao (Samatta)
Samatta anayevaa jezi namba 77 aliingia dakika ya 77 na ikamchukua dakika tano tu kupeleka kilio Club Brugge baada ya kuunganisha kwa mguu wa kulia ‘kiameizing’ mpira uliodondoshwa kwa kichwa na Malinovskyi na kufanya uwanja ulipuke kwa shangwe.

Magoli mengine ya KRC Genk yalifungwa na Karelis dakika ya 35 kwa penati na Buffalo. Meunier na Vanaken wakacheka kwa upande Club Brugge.

Ikiwa nafasi ya tano na pointi 45, KRC Genk wamebakiza mechi mbili ambapo Jumamosi ijayo wana kibarua kingine pevu ugenini dhidi ya vidume ndago Standard Liege.


Ni mechi nyingine nzuri kwa Samatta kung’arisha nyota kwenye soka la Ulaya. Ukurasa huu unakupa pongezi na kukutakia kila la kheri katika michezo iliyobaki. 
(Stori - Nathan Mpangala. Picha - Tovuti ya Genk)