Friday, February 26, 2016

NYOTA YAMWAKIA KINDA WA KI-AFGAN, ANG'ARISHWA NA MESSI

DOGO wa Ki-Afghan, Murtaza Ahmadi (5), pichani, amekuwa gumzo mitandaoni baada ya ‘kutupia’ fuko la rambo lenye jina na namba 10 ya mcheka na nyavu maarufu duniani, Lionel Messi. Picha ya dogo ikamgusa penyewe straika huyo na kuamua kumtumia jezi ya ukweli ya Argentina.

Enezo la mtandaoni (trend) la BBC liliwezesha kufikiwa kwa kinda huyo maarufu kwa ‘shabiki mkubwa wa Messi’ huko Wilaya ya Jaghori, mashariki mwa Ghazni, Afghanistan.

 Menejimenti ya Messi ilithibitisha Alhamisi iliyopita kuwa, ilishamtumia Murtaza jezi iliyosainiwa na mshambuliaji huyo wa Barcelona na mchezaji bora wa dunia mara tano.

Akiwa na furaha tele dogo alisema, "nampenda Messi na jezi naipenda. Messi kaandika kwenye jezi ananipenda pia.”

Picha iliyomuonesha Murtaza akiwa amevaa mfuko wa rambo wenye rangi za timu ya Taifa ya Argentina; bluu na nyeupe ilipata maenezo (trend) makubwa mitandaoni baada ya kuvutia watu wengi duniani.

Hatimaye ikajulikana kuwa dogo ni M-Kurd wa Iragi. Kupitia Unicef, Messi ambaye pia ni balozi wa taasisi hiyo, alimtumia Murtaza jezi aliyoisaini na kutupia maneno kadhaa ya salamu.

Pia Messi alituma jezi kadhaa ambapo sasa familia itakuwa inatinga mara moja moja akiwemo kaka wa wa dogp,  Hamayon ambaye ndiye aliyeposti picha ya mdogo wake ‘iliyokamata’ mtandaoni.

Haikuweza kufahamika mara moja nini hatma ya jezi ya zamani ya dogo ambayo kwa sasa hapana shaka imebaki historia. 
(Chanzo: http://www.bbc.com)