Friday, February 26, 2016

NGULI WA MUZIKI KASSIM MAPILI HATUNAE TENA


MWANAMUZIKI mkongwe nchini, Mzee Kassim Mapili (aliyetupia pama) amefariki dunia. Taarifa ya kifo hiko iliyothibitishwa na Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania, Bw. Addo November imesema, mkongwe huyo alikutwa na umauti chumbani kwake Tabata Matumbi, Jijini Dar es Salaam.

Bw. November alisema mwili wa marehemu ulikutwa chumbani kwake jana baada ya majirani kuingiwa na wasiwasi wa kutoonekana kwake na kuamua kuvunja mlango.

Marehemu alikuwa kiongozi wa kwanza wa kuongoza Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA). Atakumbukwa kwa vibao vyake vilivyotamba enzi hizo mfano; Mzee "Napenda Nipate Lau Nafasi" na "Rangi Ya Chungwa" na vingine nyingi.

Bw. November alisema mara ya mwisho Marehemu alionekana akiongoza wanamuziki katika mazishi ya mwanahabari nguli, Marehemu Fred Mosha katika makaburi ya Kinondoni, Jijini Dar es salaam ambako aliimba beti kadhaa za kumuenzi.

Bw. November ametoa wito kwa wanamuziki kujitokeza kwa wingi kumpa heshima marehemu. Alisema taarifa zaidi zitatolewa na kwa mawasiliano zaidi anapatikana kupitia namba 0744150000.