Sunday, February 28, 2016

MBWANA SAMATTA KUWAVAA CLUB BRUGGE LEO, KILA LA KHERI

LEO ni nafasi nyingine kwa mshambuliaji Mbwana Samatta kuthibitisha kuwa KRC Genk hawakukosea kumvuta kikosini wakati timu yake itakaposhuka dimbani kupepetana na vinara wa ligi ya Ubelgiji, Club Brugge.

Kocha wa KRC Genk, Peter Maes, amesema mchezo wa leo hautabiriki. ‘Brugge ni watamu, wana wachezaji wanyumbufu. Itakuwa ni mchaka mchaka dakika 90,’ amesema Maes.

‘Tutacheza mchezo wa kufunguka. Msimu huu hatujacheza vizuri dhidi ya timu zilizo juu. Tumekamuana nazo lakini matokea hayakuwa mazuri ’ amesema Maes.

Mpaka sasa Samatta ameshacheza jumla ya dakika 60. Dakika 15 dhidi ya Mouscron, 15 alipowavaa Beveren na 30 dhidi ya Lokeren. Kwa kiwango alichoonesha, ana nafasi kubwa ya kuingia mapema au hata kuanza.

Mechi hiyo itakayopigwa saa 8.30 mchana kwa saa za Ubelgiji, inazikutanisha timu zilizokatika kundi la wawania ubingwa. Brugge wanaongoza ligi wakiwa washavuna pointi 58 ili hali KRC Genk wana 42. Kwa mazingira yalivyo KRC Genk watahitaji ushindi kwa kila hali. (Chanzo: Tovuti mbalimbali)