FISI MADOA: BINGWA WA MIZOGA, MTAALAMU WA VICHEKO
Fisi madoa, kiumbe mroho wa nyama, hakuna ubishi katika hilo, ni mmoja
wa wanyama wanaopatikana sehemu nyingi Afrika, Tanzania ikiwemo.
Baadhi ya maeneo Afrika, fisi amekuwa akichangia makazi na binadamu.
Inadaiwa Misri, fisi alifugwa kama mbuzi, alipigwa misosi ya nguvu kisha akageuzwa
kitoweo safi. Fisi nae hakumbakiza binadamu, mpaka leo hii, binadamu akimpitia
fisi vibaya mawili, ama binadamu atageuzwa lanchi au atamegwa angalau kiungo.
Kimaumbile fisi jike kajazia zaidi ya dume, tena haswa. Ni ngumu
kutofautisha jike na dume kwa sababu, viungo vya uzazi vya nje vya jike ni sawa
na vya mumewe! Kwa lugha nyepesi dume na jike wote wana ‘tumbaku’, tofauti ni
kwamba ya jike ni kama pambo tu.
Mazingira
Kimaisha fisi madoa anaishi kwenye nyasi fupifupi, vichaka, katika
kingo za misitu, na maeneo mengine yafananayo na hayo.
Tabia
Fisi madoa huishi kiukoo, hawana masihara katika hilo. Koo hizi huwa
na ikulu zao. Ukiona eneo lina mashimo huku watoto wao wametulizana, ujue
ushaingia stetihousi ya fisi madoa. Anga hizo usipokuwa makini, ghafla waweza jikuta huna mkono au
kalio.
Fisi madoa ni bingwa wa kuweka alama kwenye himaya yake. Huweka alama
kwa kutumia kinyesi na matirio fulani yenye harufu kali nyasini kuzunguka eneo
linalomilikiwa na ukoo. Inadaiwa matirio anayotumia kuweka alama huiweka kwa
kutumia haja kubwa. Mh, fisi bwana!
Fisi madoa ni wanyama wanaopenda sana maisha ya kushirikiana. Huwasiliana
kwa kutumia miito, ishara na mapozi. Hutumia miito kama ishara kwa wenzake kuwa
eneo alilopo kuna samsingi yaani kitoweo.
Fisi madoa huzaa mpaka watoto wanne, maajabu ni kwamba, watoto wa fisi
madoa huzaliwa macho yakiwa waziiiii. Mambo ya kufumbafumba wao hawana taimu
nayo. Mtoto wa fisi madoa akishafikisha miezi mitano huanza kukata vipande ya
nyama kama madingi zao japo hunyimwanyimwa nyama mpaka wafikishe miezi kati ya 12
mpaka 18! Ni kipindi kirefu sana kwa wanyama wapenda nyama kama fisi.
Tofauti ilivyo kwa mbwa mwitu, fisi madoa yeye akipata kitiweo,
hukifyagia juu kwa juu. Watoto chakula yao ni chuchu tu. Nyama haiwahusu.
Watoto wa fisi madoa huanza kuonja tamu ya nyama wanatimiza mwaka kwani nao hujoini
misafara ya kwenda mawindoni. Ila kwa taarifa yako, usije ukapita kwenye shimo
ya fisi madoa ukaona kimya ukadhani wako watoto peke yao, hapana, ukoo ukidamka
kwenda mawindoni, fisi madoa hubaki kulinda watoto. Ukijipendekeza umeumia.
Makulaji
Fisi madoa ni mtaalamu wa mawindo, bingwa wa mazali na uporaji. Taya
lina meno makali, ana tumbo lenye mtambo mkali wa kusaga chakula ambalo
humwezesha kula ngozi, nyama na mifupa yake. Vitu ambavyo fisi madoa akila
huumpa shida ni; nywele, pembe na kwato – kwa tumbo lake haliwezi kuvisaga, hujisaidia
vikiwa viduara vidogodogo. Kiasi kikubwa cha mifupa alacho fisi madoa
humsababishia kinyesi chake kuwa kama chokaa nzito nyeupeeeee.
Maadui
Kwa kipindi kirefu fisi madoa amekuwa na mgogoro mkubwa na ongezeko la
binadamu. Isitoshe mababu wa kiafrika wamekuwa wakimhusisha ankal fisi madoa na
masuala ya kishirikina. Kama walivyo wanyama wala nyama wengine, vita vya fisi madoa
na binadamu huongezeka zaidi pale fisi madoa anapokuwa ametafuna mifugo.
(Chanzo: Mitandao)