Thursday, July 19, 2012

UJUE MFUKO WA AFYA YA JAMII (CHF)

Je, nini maana ya Mifuko ya Afya ya Jamii na uhusiano wake naa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya?

CHF ni Mfuko wa Afya ya Jamii, ulioanzishwa kisheria kupitia Sheria Na 1 ya mwaka 2001 (SURA 409 ya Sheria za Tanzania) ili kutoa huduma za matibabu kwa jamii iliyopo katika sekta isiyo rasmi mijini na hasa vijijini katika ngazi ya halmashauri, tarafa kata na kijiji.

Ni utaratibu wa hiari unaoiwezesha kaya kupata huduma za matibabu kwa mwaka mzima kwa kuchangia mara tu kiasi cha shilingi 5,000/= au 10,000/= kwa kadiri jamii yenyewe katika halmashauri husika itakavyoamua.

Serikali kwa upande wake inachangia kwa kiwango ambacho kaya inachangia hivyo kuufanya Mfuko huu kujulikana pia kwa jina la Tele kwa Tele.  

Mfuko huu ulianza kwa majaribio wilayani Igunga mwaka 1996 na baadaye kuenea katika Halmashauri mbalimbali nchini ijapokuwa kasi yake imekuwa sio ya kuridhisha. Mwaka 2007 Serikali iliamua kuwa Shughuli za Mfuko huu na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ziwianishwe.  

Hatua hii ilisababisha Serikali kuu mwezi Juni 2009 kukasimu mamlaka yake kitaifa ya kusimamia na kuendesha CHF  kuwa chini ya NHIF wakati Halmashauri zikiendelea na majukumu yake ya awali.  

Uamuzi huu unalengo la kuwezesha kutekeleza kwa kasi Mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi (MMAM 2007-2017), kuongeza uwigo na kuenea kwa CHF katika Halmashauri mbalimbali na pia kuboresha huduma ngazi ya Zahanati na Vituo vya Afya kwa sababu huduma zinazotolewa katika ngazi hizo zinawanufaisha wanachama wa Mifuko yote miwili.

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ambao ndio wasimamizi wakuu wa CHF kitaifa, kiutaalamu na kiutawala waliona ni vyema kutumia uzoefu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, NHIF, na baraza la mawaziri liliagiza kukasimishwa madaraka ya kuratibu mifuko hiyo NHIF kwa lengo la kuoanisha shughuli zao, kuboresha huduma na kuongeza uwigo wa wananchi wanaohudumiwa na CHF hasa vijijini. Blogu hii itakuwa ikiwalete dondoo mbalimbali kuhusu mifuko hii kila wiki. Usikose.