Saturday, May 05, 2012

WABUNGE WATEULE WANENA

Saturday, 05 May 2012 10:25
Mh. Janet Mbene
Fidelis Butahe
WABUNGE wateule  wamesema ili kuepusha mvutano baina ya serikali na jamii viongozi nchini wanatakiwa kuwajibika na kuwa karibu zaidi na wananchi huku mmoja wao, Profesa  Sospeter Muhongo akisita kuzungumza kuteuliwa kwake kwa sasa na kufafanua kuwa wanasayansi siyo wanasiasa.

Wabunge hao walioteuliwa juzi na Rais Jakaya Kikwete ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Sospeter Muhongo, kada wa CCM, Janet Mbene na Saada Mkuya.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, Mbene ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi ya chama hicho jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Masaki alisema yupo tayari kuwatumikia wananchi  kwa kuwa ni mzalendo.

Mbene ambaye aliwahi kuteuliwa na rais kuwa mbunge Februari 2010 alisema,  viongozi wana wajibu wa kuwa karibu na wananchi ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha na kuwasikiliza matatizo yao.

“Tusipofanya hivyo wananchi wanaweza kuhisi  lolote, inawezekana haya yaliyotokea kwa mawaziri yametokana na mambo kutowekwa wazi na kutolewa ufafanuzi, wananchi wanatakiwa kupewa ufafanuzi wa masuala mbalimbali, pia wapewe huduma muhimu malalamiko yatapungua,” alisema Mbene.

“Ukiwa waziri kazi hufanyi peke yako unakuwa na wasaidizi, pia wapo wenzako ambao utawakuta na wana uzoefu kwa hiyo kwangu haitakuwa kazi kubwa kwa nafasi hii niliyopewa ya naibu waziri wa Fedha, unapopata fursa kama hizi unatakiwa kutumia ulichonacho kwa ajili ya wengine” alisema Mbene.

Mbene aliyewahi kugombea ubunge wa viti maalum kupitia NGO mwaka 2010 lakini alishindwa na Rita Mlaki. Hivi karibuni aliteuliwa na Kamati Kuu (CC) ya CCM kuwania ubunge wa Afrika Mashariki lakini alishindwa baada ya kupata kura chache katika uchaguzi uliofanyika Bungeni, Dodoma.

Kwa upande wake Mbatia alisema kuwa ameteuliwa na rais kuwa mbunge kutokana na chama chake kuwa na siasa za kujenga hoja, siasa  ambazo zinawafanya watanzania kudai haki zao bila vurugu na kumwaga damu.

Alisema kuwa hajachaguliwa kwa upendeleo wala kulipa fadhila na kwamba Rais Kikwete amefanya uteuzi huo kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

“Katiba iko wazi na imeeleza kuwa Rais anaweza kuteua mtu yoyote bila kujali anatokea chama gani cha siasa. Katika suala zima la uongozi hakuna mwenye hati miliki ya kuwaongoza watanzania” alisema Mbatia

Mbatia ambaye Januari 21 mwaka huu akiwa na viongozi wengine wa chama hicho waliitwa Ikulu kutoa maoni yao kuhusu Katiba mpya alisema tatizo kubwa linaloikabili nchi ni mfumo wa elimu ambao unasababisha mmonyoko wa maadili, ukosefu wa uadilifu na uaminifu, uwajibikaji wa pamoja na watu kutopenda kufanya kazi.

“Mfumo huu unawafanya watu kutoiheshimu Katiba na sheria za nchi jambo ambalo linasababisha kuwapo na pengo kubwa kati ya mwenye nacho na asiyenacho” alisema Mbatia.

Alisema kwa kuwa amechaguliwa kuwa  mbunge  jukumu lake kubwa ni kuwatumikia watanzania wote na sio wa  chama chake pekee.

Wakati Mbatia akieleza hayo  Profesa, Sospeter Muhongo aliyeteuliwa kuwa waziri wa nishati na madini alisita kuzungumzia uteuzi huo na kusema kuwa wanasayansi sio wazungumzaji kwa kuwa sio wanasiasa.

Profesa huyo wa Jiolojia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,  Profesa wa heshima wa Jiolojia katika Chuo Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini aliombwa atafutwe siku nyingine na kuahidi kuwa atazungumza kwa kirefu kuhusu kuteuliwa kwake.

Huku akizungumza kwa furaha alisema, “Nisamehe kijana wangu unajua wanasayansi si wazungumzaji sana kwa kuwa sio wanasiasa, nipe muda kidogo nakuahidi kuwa tutazungumza mengi tu ila kwa sasa nipe muda”.

Wasifu wao
Mbatia mbali na kuwa Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, kitaaluma ni mhandisi na aliwahi kusoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kati ya mwaka 1987 hadi 1992 alipofukuzwa kutokana na migomo iliyotikisa chuo hicho .

Baadaye mwaka 2007 hadi 2009 alikwenda nchini Uholanzi kusomea International Civil Engineering akibobea zaidi katika eneo la kukabiliana na majanga (Risk management).

Mbatia pia amewahi kuwa mbunge wa Vunjo na amekuwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi tangu Machi 6, 2000 na uongozi wake unatarajiwa kukoma mwaka 2013.

Naye Janet Mbene ana Shahada ya Uzamili ya Uchumi kutoka Chuo cha New England Australia. Ni Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Kampuni binafsi ya SIA, ambayo inajenga uwezo kibiashara kwa kampuni ndogo na za kati.

Amewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ikiwamo Umoja wa Mataifa (UN), Shirika la kimataifa la Oxfam, Programu ya Maendeleo ya UN, Shirika la Kazi la Kimataifa na mashirika ya kimataifa yasiyokuwa ya kiserikali.

Pia ni mwanzilishi na mwenyekiti wa Shirika la Yatima Trust linaloshughulika na masuala ya wagonjwa Ukimwi na kutoa msaada kwa watoto yatima.

Ni mwanazuoni wa Heshima katika jumuiya kadhaa za kimataifa na kwa sasa ni Makamu wa Rais wa Tume ya Ramani na Jiolojia Duniani (CGMW) na Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU) inayoshughulikia utoaji wa Tuzo za Kisayansi za Kwame Nkrumah kwa ajili ya wanasayansi bora iliyoundwa mwaka 2011.

Profesa Muhongo pia ni Mhariri Mkuu wa Jarida la Afrika Dunia Sayansi (Elsevier), Msaidizi wa Mhariri wa Precambrian Utafiti (Elsevier) na mwanachama wa bodi kadhaa za wahariri wa majarida ya kisayansi.

Alikuwa Rais wa Chama cha Geological ya Afrika (1995 - 2001) na Mkurugenzi mwanzilishi wa Kanda (2005 - 2010) wa Ofisi ya ICSU ya Mkoa kwa ajili ya Afrika, Pretoria, Afrika Kusini.

Alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya masuala ya kisayansi wa UNESCO mwaka 2004 - 2008, na Mwenyekiti wa Programu ya Sayansi ya Kamati (SPC) ya Mwaka UN-kutangazwa Kimataifa wa Sayari ya Dunia ( IYPE) 2007 - 2010.

Kazi zingine alizowahi kufanya ni pamoja na kuwa Mwenyekiti  wa Bodi ya Wakurugenzi wa State Mining Corporation (STAMICO) na Mkuu wa Idara ya Jiolojia, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (1997-2000).

Prof Muhongo alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Serikali ya Tanzania ya Uchunguzi wa ajali ya wachimbaji madini ya Tanzanite Mererani iliyotokea mwaka 2002. [Chanzo: www.mwananchi.co.tz]