Tuesday, May 01, 2012

NIKUJUAVYO KOMRADE FRANK ODOI (3)

* Umeondoka lakini kazi zako zitaendelea kuishi

KOMREDI wangu, Frank Odoi, umejizoelea umaarufu nchini Kenya kwa katuni yako ya Driving Me Crazy ambayo kimsingi ilikuwa inawalenga madereva wa matatu ambao wanasifika kwa uendeshaji rafu nchini humo. Hao hao, Jumamosi ya tarehe 22.4.2012, ukiwa na miaka yako 64 tu, wakachukua uhai wako kaka, tena kirahisi tu!

Hata Mugabe atakukumbuka
Veteran, ulikuwa maarufu kutokana na komiki yako ya Golgoti, inayomhusu mtasha aliyetembelea Afrika na jamaa mmoja jasiri toka Afrika ambaye alikuwa akivutiwa na simulizi za zamani toka Ghana, nchi yako ya asili.

Baada ya kumaliza masomo yako ya sanaa na ubunifu huko kwenu Accra, miaka ya 1970, Komredi Odoi ulitimkia Kenya na kuweka makaazi na kuwa miongoni mwa wachoraji ambao kazi zenu zilikuwa zinapamba gazeti la Daily Nation kwa sana.

Katuni hii itaendelea kuishi
Komredi Odoi, kazi zako zimesambaa nchi mbalimbali kaka. Uganda, Ghana, Msumbiji, Denmark, Finland na jarida la BBC Focus on Africa kote huko wanafaidi sanaa yako. Umefanya maonesho ya komiki na katuni sehemu mbalimbali duniani na kujizolea tuzo kadhaa.

Ama hakika umeacha pengo kubwa kwenye taaluma hii hapa Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla.

Mkono wa Mwalimu wangu, Komredi Odoi
Akinukuliwa afisa mmoja wa trafiki, Patrick Lumumba, alisema, Komredi Odoi ulipanda matatu, wakati mko njiani, dereva alijaribu kumkwepa mwenda kwa miguu aliyekuwa akikatiza barabara, basi likapinduka na kutua msingini na kuuwa abiria wawili ukiwemo wewe Komredi wangu, Odoi!

Komredi Odoi, baada ya kutoonekana nyumbani wikendi nzima, familia yako iliingiwa na wasiwasi, sana tu. Walihaha kukutafuta kila hospitali, hatimaye wakakukuta umefumba macho, umewekwa mochuari katika moja ya hospitali, jijini Nairobi. Inauma sana.

Komredi Odoi, nitaendelea kutumia elimu ya uchoraji uliyonipa. Kazi zako zitaendelea kuwa kichocheo cha kazi yangu. Utabaki kuwa komiki artisti na katunisti wangu wa mfano. Umetangulia, lakini kazi zako zitaendelea kuishi.
Komredi Odoi anatarajiwa kuzikwa Jumamosi, Mei 5, Kenya.
Daima nitakukumbuka, Komredi Frank Odoi.
Amen.