Monday, May 07, 2012

MAMA PINDA APOKEA MICHANGO YA SHILINGI MILIONI 16

MKE WA WAZIRI MKUU, Mama Tunu Pinda, leo amepokea michango kutoka kwa kampuni za Vocacom na Zantel ikiwa ni mwitikio wa ombi lake kwa Watanzania kuwaomba waichangie timu ya Taifa ya Netiboli (Taifa Queens).

Mama Tunu Pinda, amepokea vifaa vya michezo kwa ajili ya mashindano kutoka kampuni ya Vodacom Tanzania vyenye thamani ya  sh. milioni sita. Vilevile, Mama Pinda  amepokea simu za mkononi 300 zenye simcard na muda wa maongezi kwa ajili ya wachezaji na viongozi wao kampuni ya Zantel zenye thamani ya  sh. milioni 10/-. 
Makabidhiano hayo yalifanyika leo mchana (Jumatatu, Mei 7, 2012) kwenye makazi ya Waziri Mkuu Oysterbay, jijini Dar es Salaam.
Akikabidhi vifaa hivyo vya michezo hiyo, Meneja Mahusiano ya Nje wa VODACOM, Bw. Salum Mwalimu alisema wameitikia wito wa Mama Pinda wa kuichangia timu ya Taifa Queens kwa sababu wametambua umuhimu wa kuiunga mkono timu hiyo. 
“Vifaa tulivyotoa ni jezi 20, tracksuit 20, raba pea 20 na bibs 20… tuna imani timu yetu ya taifa itaweza kupenya hadi ngazi ya fainali,” alisema.
Naye Meneja Biashara wa Zantel, Bw. Ahmed Mokhles akikabidhi simu hizo, alisema wametoa mchango huo kwa sababu wanaamini kwamba japokuwa watakuwa hapa nchini, wachezaji na maafisa wao wana haki ya kuwasiliana na familia zao.
“Kwa kutambua hilo, tumetoa simu 300 zenye muda wa maongezi ambapo mtu akiongeza muda wa maongezi, ataongezewa muda mwingine wa sh. 10,000/- kila mwezi kwa muda wa miezi mitatu.”
Pia Zantel walitoa router mbili kwa ajili ya ofisi za Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) ili ziweze kuwasadia katika mawasiliano yao ya internet.
Mama Tunu Pinda aliwashukuru makampuni yote mawili kwa michango yao, na akatumia fursa hiyo kuwashukuru zaidi Watanzania waliojitokeza kwa wingi kuchangia mashindano hayo.
Akitoa ufafanunuzi kuhusu michango ambayo imekwishatolewa hadi sasa, Mama Pinda alisema jumla ya sh. 178,230,000/- zimekwishapokelewa hadi sasa zikiwa ni fedha taslimu na vifaa. Kati ya hizo, sh. milioni 114.8 ni fedha taslimu na sh. milioni 53.4 ni vifaa vilivyotolewa na wadau mbalimbali kuchangia mashindani hayo.
Alisema bajeti nzima ilikuwa sh. 158,439,000/- ambapo sh. 82,656,000 zilikuwa ni gharama za kuendeshea kambi ya maandalizi ya timu ya Taifa Queens na sh. 75,780,000/- zilikuwa ni kwa ajili ya kuendesha mashindano yanayotarajiwa kuanza kesho.
Tanzania kupitia CHANETA imepewa heshima ya kuandaa Mashindano ya Netiboli ya Kombe la Afrika ambayo yanatarajiwa kuanza kesho saa 8 mchana (Jumanne, Mei 8-12, 2012). Mashindano hayo yanayojumuisha nchi saba za Botswana, Lesotho, Zimbabwe, Zambia, Uganda, Malawi na Tanzania yatafunguliwa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete.
Mke wa Waziri Mkuu, Bi.Tunu Pinda pamoja na Kaimu Katibu Mkuu wa Chaneta, Bi. Rose Mkissi, wakipokea vifaa vya michezo kwa ajili ya timu ya taifa ya Netiboli -  Taifa Queens kutoka kwa Meneja wa Mahusiano ya Nje wa Vodacom Bw. Salum Mwalim. Vodacom imeipatia Taifa Queens vifaa mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni sita kuwezesha ushiriki mzuri wa timu hiyo kwenye mashindano ya Afrika yanayoanza kesho (Jumanne Mei 8, 2012) Jijini Dar es salaam. Wa kwanza kulia ni mjumbe wa kamati ya maandalizi ya mashindano, Bi. Shiza Mwakatundu. [Stori/Picha kwa hisani ya Blogu ya Fullshangwe]