Wednesday, May 09, 2012

MAKUMBI JUMA ALIKUWA ‘HOMA YA JIJI’ KWELIKWELI

- Simba ndio waliompachika jina ‘Homa ya Jiji’
- Ashangaa wageni kung’aa ligi kuu
- Adai washambiliaji wetu ni butu, hawatulii golini

ALIKUWA ni mmoja wa washambuliaji hatari wa klabu ya Yanga na timu ya taifa, Taifa Stars, kuweza kutokea katika historia ya soka la Tanzania. 

Huyu ni Makumbi Juma au ukipenda 'Homa ya Jiji,' jina alilopewa na mashabiki wa Simba kutokana na uwezo wake mkubwa wa kupachika mabao. Aliwapa presha watani wao wa jadi wakati wote wa mchezo na wakati mwingine walikuwa wakiomba asichezeshwe au awe mgonjwa.

"Ni Simba walionipa jina la 'Homa ya Jiji' kwa sababu nilikuwa nawapa presha na kuwafunga magoli muhimu," anasema.

Makumbi,55, alizaliwa katika mji wa Uvinza unaozalisha chumvi kwa wingi Mkoani Kigoma. Alipenda sana kucheza soka tangu akiwa shuleni. "Shuleni kulikuwa na vipindi vya michezo kama riadha, kuruka juu na soka ambayo niliipenda sana kushiriki," anafafanua.


 Baada ya kumaliza masomo 1977 mchezaji huyo alijiunga na timu ya Mamlaka ya Pamba Kigoma, ambako alikutana na wachezaji kama Khalid Bitebo, Abuu Juma, Ali Katolila, Rajabu Mhoza na wengineo.

Abuu Juma ni kaka wa Makumbi Juma ambaye aliwahi kuchezea klabu ya Simba na Taifa Stars. 'Homa ya Jiji' aliichezea Pamba Kigoma kwa msimu mmoja.


Pamba Kigoma ni timu ambayo iliwahi kuwa tishio katika Ligi Daraja la Kwanza, ambayo ilikuwa ikiendeshwa kikanda. Ni katika ligi hiyo Yanga walimuona Makumbi na kuvutiwa na uchezaji wake.

Makumbi alijiunga Yanga rasmi mwaka 1980 na kukutana na wachezaji mahiri kama Hamis Kinye, Ahmed Amasha, Charles Boniface 'Mkwasa' na wengineo.

"Hakika nilijisikia furaha sana nilipojiunga Yanga kwa sababu ni moja ya klabu kubwa hapa nchini. Imenifanya nifahamiane na watu wa aina mbalimbali na kuishi nao vizuri," anasema.

Makumbi, ambaye aliichezea Yanga kwa mafanikio makubwa kwa takriban miaka 10, mechi yake ya kwanza ya kimataifa akiwa klabu hiyo ni dhidi ya Rio Tinto ya Zimbabwe.


Yanga walikumbana na Wazimbabwe hao katika mashindano ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati mwaka 1981. Yanga walishinda 2-0. Makumbi alifunga goli moja na lingine kufungwa na Abeid Mziba, ambaye alikuwa kama pacha wake kwani akifunga na yeye lazima afunge.

"Uwezo wangu ulikuwa mkubwa ndo maana nilikuwa nachukua namba Yanga iliyokuwa imesheheni mastaa," anasema kwa kujiamini.

Makumbi aliichezea timu hiyo ya Jangwani mechi nyingine nyingi za kimataifa ikiwemo dhidi ya Nkana Red Devils ya Zambia.

Pia alitisha dhidi ya Gor Mahia ya Kenya iliyokuwa na wachezaji kama John Bob Ogola, Wilberforce Mulamba na Dr. J.J. Masiga, ambaye ni daktari wa meno.   


Makumbi alichaguliwa Taifa Stars 1980 na mechi yake ya kwanza ya kimataifa ambayo hataisahau maishani mwake ni dhidi ya Malawi.
Anaikumbuka kwa sababu Malawi iliundwa na wachezaji makini kama Jack Chamangwana, Kinnah Phiri na Young Chimodzi, ambao aliwasumbua ingawa Malawi ilishinda 2-1.    

'Homa ya Jiji' alikuwa akicheza namba 9 au 10. "Ukiwa mshambuliaji ni lazima ubadilibadili namba mabeki wasikuzoee," anazidi kutoa somo. 

Anakumbushia enzi zao upinzani wa Yanga na Simba ulikuwa mkali sana kwani shamrashamra zilitangulia karibu mwezi mzima huku bendera zikipachikwa kwenye miti na magari.

Anasimulia mashabiki waliweza kutoka mikoani kuja kuangalia mechi na vituko vilikuwa vingi uwanjani kama kuvaa vinyago na kurusha njiwa.

Anaikumbuka mechi ya Yanga na Simba, ambao walitoka mafunzoni Brazil walikokaa kwa miezi mitatu na kurudi na staili ya 'diagnal.'

Mechi hiyo ilijaa mashabiki wengi wakitaka kuiona Simba imejifunza nini Brazil. Walifurika uwanjani kuanzia asubuhi wakishindia maji na rambaramba (ice cream).

Hata hivyo, siku ya siku ni Yanga walishinda 3-1, Makumbi akifunga goli la kwanza, Abeid Mziba la pili na latu likihitimishwa na Omar Hussein 'Keegan.' 


 Mechi ilikuwa ya kusisimua na yenye ufundi mwingi kwa pande zote mbili huku mashabiki walitamani isimalizike haraka. Anasema Mohamed Bakar 'Tall' na Athuman Juma ni mabeki wa Simba waliokuwa wakimpa taabu ingawa walikuwa ukingoni kutundika daluga.

Hata hivyo, anasema Lilla Shomari na Filbert Lubibira kutoka mkoa wa Kagera ni mabeki wa Simba waliomsumbua zaidi kutokana na kucheza 'dabo sentahafu.'

Anamsifia kocha mzawa, Mohamed Msomali, kwamba ni kocha bora aliyefundisha wachezaji wengi kwa mafanikio na ni wachache wenye uwezo kama wake.

"Msomali ni kocha anayeweza kumbadilisha mchezaji namba na kucheza kwa mafanikio ni wachache sana wanaoweza kufanya hivyo,"

Makumbi, mwenye mke na watoto watatu wa kike, Matama, Sharifa na Johari, anasema soka letu linazidi kudidimia 'hata ukiangalia kwa macho.'

"Wachezaji wa sasa hawajitumi si kwa Stars pekee, hata kwenye klabu zao. Kama hujitumi kwenye klabu yako ni dhahiri hata timu ya taifa utafanya vivyo hivyo," anafafanua.

Anabainisha kwamba wachezaji wetu leo wakimwona kocha wa kigeni anakuja na mazoezi magumu wanamwona ni adui na kumfanyia mizengwe kama vile kucheza chini ya kiwango na hatimaye kubwaga manyanga.

Anawaasa wachezaji wa sasa kupunguza starehe kwani soka linahitaji nidhamu ya hali ya juu na mchezaji kamwe hawezi kuwa kwenye kiwango kama atakwepa mazoezi magumu.


Pia anasema soka letu linazidi kwenda arijojo kwa sababu uongozi wa soka (TFF) umezongwa na watu (wafanyabiashara) ambao hawana mapenzi na mchezo huo.

Kitu kingine kinachochangia kushuka soka letu ni wahisani kupendelea kufadhili Simba na Yanga badala ya klabu ndogo kama Toto Afrika ambazo ndizo zenye vipaji.

Anasema hii yote ni kutokana na madudu ya soka letu na ndiyo maana wapenzi wengi wa Bongo wanashabikia timu za Ulaya. Anasema hata enzi zao timu za Ulaya zilikuwepo, lakini kwa sababu wao walikuwa wanacheza vizuri mashabiki walikuwa hawazishobokei kama ilivyo sasa.

"Naweza kutembea barabarani hivi leo na mchezaji wa Stars, lakini wapenzi wa soka watanishangilia mimi kwa sababu kiwango changu kilikuwa juu," anasema.

Anazidi kukosoa wachezaji wa sasa hawataki kujifunza, hawajitumi na hawana wivu wa maendeleo na ndio maana wanashindwa kupafomu.

"Nashangaa mchezaji bora anakuwa Mwape au Asamoah akiwa na magoli tisa halafu mzawa ana magoli mawili na kila mechi amekuwa akipangwa. Huyu mzawa hawezi kujiuliza kwa nini inakuwa hivyo?"

"Mastraika wetu ni butu sana, wanashindwa kutulia wanapofika golini. Straika hapaswi kuwa na wasiwasi, bali kutulia na kufunga goli," anazidi kusema.

Kwa sasa Makumbi Juma anafundisha timu ya Mantare Rangers ya Mwanza ambayo inashiriki ligi ya mkoa huo. Ni 'Homa ya Jiji.'