Friday, May 11, 2012

JIWEKE KWENYE NAFASI YA MZAZI HALAFU SOMA KIPANDE HIKI

KIJANA mmoja aliweka kipande cha karatasi chenye ujumbe chumbani kwa madingi zake kikiwa na haya yafuatayo;


Baba na mama ni matumaini yangu kuwa mtasoma ujumbe wangu huu kwenye karatasi niliyoiweka juu ya meza. Nawaombeni msishtuke maana ni mambo ya kawaida tu kwenye maisha tunayoishi.

Whaaat!

Najua mtaumia kwa vile bado nasoma na ndo kwanza nipo kidato cha kwanza. Napenda kuwajulisha kwamba sasa hivi mnapoisoma barua hii, sipo nyumbani, nimetoroka. Nimegundua nina uwezo wa kujitegemea kwa sababu mimi ni kijana mwenyewe umri wa miaka 14, najua zuri na baya.

Tangu mwezi mmoja uliopita, nimekuwa na uhusiano na dada mmoja aliyeitwa Roda, mwenye umri wa miaka 37. Tunaishi pamoja kwenye chumba tulichopanga karibu na makaburi ya maji machafu.

Nilipokuwa nyumbani sikuwa napata hela zaidi ya alfu moja moja mlizokuwa mkinipa. Ila sasa nimeanza kushika noti za shilingi elfu kumi kumi, nainjoi kwa kweli. Mchumba wangu ni mrembo, mama hafui dafu.

Roda amenifundisha njia za kutafuta hela. Amenipa mchongo wa kuuza ‘unga’. Yeye kabobea kazi ya uuzaji viwanja hewa hapa jijini. Ni mtaalam kweli kweli. Aliniambia ana digrii ya kuzaliwa nayo. Sio siri, kama ni hela tu tunazichanga.

Mchumba wangu ana bidii sana ya kufukuzia hela. Kila siku analala masaa matatu. Mteja akija tu atahakikisha anazunguka nae mtaani mpaka amchomoe mavumba.

Msiwe na hofu, nipo salama kabisa na nimeamua kumwoa Roda maana ni kila kitu kwangu.
Pia amenunua mchuma wa kubebea kuni na biashara inaenda vizuuuuri.

Hivi karibuni Roda alitiwa mkononi kwa kosa la utapeli, nikaenda kumwekea dhamana na sasa yuko nje. Juzi aliniambia ili kesi ife inabidi nifanye juu chini nimkabidhi hati ya nyumba mliyojenga, hilo nimetimiza jana.

Kwa kuwa nimekufa na mahaba ya mchumba wangu, inabidi nimridhishe kila kitu. Huwa nafanya naye mazoezi ya viungo, namchomolea hela toka kwenye akaunti ya baba na tukialikwa harusini huwa ananiambia nitumie suti za baba kisirisiri.  Si mnajua tena unapopenda unakuwa huambiliki. Sio inakuwa ndio, ndio inakuwa sio.

Tumepanga tutawatembelea baada ya miaka 10. Natumaini muda huo ukifika tutakuwa na watoto wanne hivi. Tutawaleta wajukuu mkakae nao kwa sababu Roda anasema, hatoweza kulea watoto. Wazazi wangu sina la kuongeza, kwaherini. Mungu akipenda tutaonana.

Baba na mama, mimi nipo chumbani kwangu. Mnachokisoma ni home work. Mwalimu wa kiswahili ametupa leo, katuambia tutunge hadithi fupi. Naomba muipitie muone kama ina makosa ili Jumatatu niipeleke shule.