Wednesday, May 09, 2012

DALADALA SASA NI MIN BUZZ, LIVE PALE PALE TBC1

WATAYARISHAJI maarufu wa kipindi cha runinga cha ‘daladala’ leo wamezindua upya kipindi hiki kwenye televisheni ya TBC kikiwa na jina jipya la Minibuzz.

Minibuzz ni kipindi kinachoatayarishwa na MADE IN AFRICA TV, kampuni ya utengenezaji na utayarishaji wa vipindi ambavyo vina ujumbe kwa ajili ya jamii ya kiafrika.

Awali kilizinduliwa hapa nchini Tanzania mwaka 2010, kama daladala na kwa muda mfupi sana kilipata wapenzi wengi takribani watu milioni tatu.   Na kwa mafanikio hayo, kampuni hiyo iliweza kuzindua mfumo huo huo katika nchi ya Uganda na Kenya.

Mtayarishaji mkuu, Frank Bierens, alisema, “Jina lipya la Minibuzz linakusudia kuongeza nguvu na kuunganisha Afrika mashariki.  Kwa kufanya kazi chini ya jina moja na kushirikiana katika utayarishaji, kwa hivyo tunatarajia  kuepukana na usumbufu katika soko na kuwa wazi kwenye makusudio ya kipindi hiki”.

Minibuzz inarekodiwa kila asubuhi ndani ya gari ndogo aina ya Hiace ambayo ina muundo wa studio.  Ina camera, vinasa sauti na vifaa kwa ajili ya uhariri.  Washiriki ni abiria wa kawaida ambao hupanda basi hili katika vituo mbalimbali nchini kwa ajili ya kujadili maswala mbalimbali yanayohusu maisha yao. 

Kipindi hiki chenye jina jipya kitaendelea na watangazaji wake Daniel Kijo na Bibi Kiroboto sasa hivi kina sura mpya kabisa ya Tumaini Meshack.

Watayarishaji wa vipindi wa MADE IN AFRICA TV –wametangaza uzinduzi wa kipindi cha Radio cha Minibuzz kitacholetwa kwenu na Bibi Kiroboto akishirikia na Daniel Kijo na Tumaini Meshack. Mfumo huu mpya unakusudia kuleta mwamko kwa wapenzi na wasikilizaji nchini.

Daniel Kijo amesema, “Nina furaha kubwa kwa kuzinduliwa kwa kipindi hiki, kama awali hii ni nafasi ya mtu wa kawaida kabisa kusikika na kuleta changamoto ya mabadiliko Tanzania.  Katika mabadiliko ya kipindi hiki, tunatarajia kuwafikia na kuwaunganisha watanzania wengi zaidi.    Kwa kufanya vipindi vya televisheni na Radio tunaleta muungano katika mipaka yote ya kijamii Tanzania.

Tumaini Meshack ambaye ni mtangazaji mpya wa kipindi cha Minibuzz amesema, ”Nimefurahi kuungana na timu hii ya Minibuzz kwani kwa muda mrefu nimekuwa mpenzi wa kipindi hiki.  Na sasa, tunatarajia kuungana na watazamaji wetu wote, katika mada tofauti muhimu za kila siku.  Ni kupitia mazungumzo au mijadala, tunaweza kuendeleza na kuboresha hali ya maisha hapa Tanzania.

Akiongezea yaliyosemwa na wenzake, Bibi Kiroboto naye alikuwa na haya ya kusema, “Mimi nimefurahi zaidi kwa kipindi cha radio cha Minibuzz kwa vile tutawafikia watanzania wengi zaidi hususani vijijini. Radio inaikika kila sehemu na wakati wowote.

Kipindi cha Minibuzz cha televisheni kinarushwa hewani kila siku katika televisheni ya TBC1 saa kumi na mbili jioni.   Kwa redio, ni kila siku saa moja jioni katika kituo cha radio cha TBCFM.

Kwa maelezo zaidi, wasiliana na Ms. Eugenia Chanda kwa simu namba 0713 548496. Au kwa barua pepe, eugeniachanda@yahoo.com

Mark Zuckieraian kushoto, Dan Kidjo anayemfuatia, Christina Mbunda na Tumaini Meshack wakizungumza na Waandishi leo kuhusu MIN BUZZ mpya. 
Mmiliki wa Blogu ya mitindo, 8020fashions.blogspot.com, Bi.  Shamim Mwasha, mwenye miwani, naye alikuwa mmoja wa shuhuda wa uzinduzi huo.