Sunday, April 29, 2012

NIKUJUAVYO KOMRADE FRANK ODOI

*Dereva wa Matatu amekatisha uhai wako

* Umeondoka, kazi zako zitaendelea kuishi

Machi 12 mwaka huu, nikiwa katika safari zangu za hapa na pale, nilipitia kwenye ofisi yenu kuwasalimia hapo Revlon Professional Plaza, ghorofa ya tatu, Biashara striiti, Jijini Nairobi. Nakumbukuka ilikuwa majira ya mchana ambapo pamoja na wewe pia nilikutana Madd na Mbongo mwenzangu anayechorea gazeti la Nation, Gado.
Komredi Frank Odoi

Pamoja na kusalimia pia nilipita ili niweze kutumia ofisi yenu kuchora vibonzo na kutuma nyumbani chapchap ambako vilikuwa vinasubiriwa kwa hamu kwa kuwa nilikuwa tayari nimeshachelewesha kazi.

Wakati natoa majembe yangu za kuchorea, nikagundua nimesahau kifaa muhimu cha kuchorea, kinaitwa pen tablet! Nikachoka. Laptop na wacom tablet (kifaa kama ubao cha plastiki cha kuchorea) nilivibeba, kivumbi kikawa hiyo ‘kalamu’. Nilikuwa nimeisahau Dar es Salaam. Nikajisemea moyoni, huu sasa msala.

Wakati nahaha nifanyeje, Komredi Odoi ukasema, nisitie shaka, unayo. Ukavuta droo na kunipa. Kasheshe nyingine ikaibuka, kalamu uliyonipa ni ukoo bamboo. Mimi natumia jamii ya wacom.
Moro, enzi hizoo! 1996, Nathan(kushoto), Odoi (katikati)
Hukuchoka komredi wangu, ukaona bora unitolee na pad yake ya kuchorea (Bamboo) kabisa. Nilipoikonekti kwenye laptop yangu nikaundua haina mawasiliano! Unajua kwa nini? Sikuwa na drivers zake. Zoezi likafa kifo cha kawaida.

Hamu ya kuchora kwa teknolojia ya kisasa ikaniisha. Nikaanza kuzikumbuka karatasi, peni na kifutio ambavyo sikubeba kwa sababu nilikuwa na uhakika kuwa niko kamili gado na kitekelinalokujia tena la kisasa, wacom tablet!

Komredi Odoi hukuishia hapo, ukanipa karatasi, penseli na kifutio juu. Wakati naendelea kuchora, ukaanza kunipa mkasa wa skana yako. Ukiongea kwa lafudhi yako Kiafrika Magharibi, ukasema; “Nathan, look at my scanner, I will tell you what happened”
Moja ya kazi za Komred Odoi

Nikaitupia jicho skana na wewe ukaniangalia, mara macho yetu yakagongana. Kama kawaida wakutanapo wachora katuni, utani huwa mwingi, tukamwaga kicheko cha nguvu. Uliishikiza mashine yako na waya pembeni! Ilikuwa imejeruhiwa lakini bado inapiga mzigo ila kwa taimingi.

Ukasema, siku za karibuni ulisafiri kwa pipa kwenda kwenu Ghana. Ulipofika kiwanja cha ndege, ‘ukacheki-ini’ mzigo wako. Unasema ulipofika mwisho wa safari, ulichukua begi lako na kuishia.
Ulipofika maskani, ulipolifungua ukachoka. Ulikuta skana iko dhoofu kulu-hali, meng’emeng’e, imesambaratika. Huku ukicheka, ukaendelea kunipa stori ukasema; “Nathan, ukisafiri usiweke kitu cha kuvunjika kwenye begi halafu ukacheki-ini, ingia nalo ndani ya ndege. Wanaodili na mizigo huwa wanarusha mabegi kama basketi bolu”. Wote tukacheka sana ukichombeza na “you see, you see..,” nyiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiingi.

Baada ya kuchora na kutuma Dar es Salaam, nikaona niwaage ili nisepe zangu. Ukinielekezea simu yako, Komredi Odoi ukasema, “Nathan, wait, wait, I want put it on my facebook page”, akimaanisha nisubiri anifotoe ili aweke kwenye peji yake fesibuku.

Komredi Odoi, leo ndio najua kumbe Machi 12, 2012 ulikuwa unaniaga rasmi.  Oh, my God!
Inaendelea Kesho