Monday, April 30, 2012

NIKUJUAVYO KOMRADE FRANK ODOI (2)

*Awatahadharisha wachora katuni kutolewa na kompyuta

*Alikuwa msheshi na mtu wa vituko

Kwa mara ya kwanza, nilikufahamu Komredi Odoi, Mji kasoro Bahari-Morogoro kwenye warsha ya wachoraji katuni mwaka 1995 iliyoshirikisha wachoraji katuni mahiri akiwamo marehemu, John Kaduma.

Mwaka uliofuatia ikafanyika warsha nyingine tena ya komiki  iliyokuwa imeandaliwa na Tanzania Popular Media Association (TAPOMA).

Komredi Odoi, nakumbuka ilikuwa kipindi cha mvua na baridi toka milima ya Uluguru ilikuwa inapuliza kisawasawa. Rafiki yangu, Francis Bonda na timu yake wao wenzetu walishajifunza kutumia maji ya mende mapemaaa.

Hivyo ilikuwa nafuu kwao kwani wakipiga mbili tatu, ilikuwa ni fulu joto. Nakumbuka nilikuwa nashea rumu na mwanangu mwenyewe,  Abdul Gugu. Tulikuwa na kanda yetu ya mchiriku, Gugu alikuwa halali bila ya kuisikiliza. Mbali na kutuliwaza pia ilikuwa inatupa mainspiresheni na mahisia. 
Hapa Komredi alijichora


Nilipata mwaliko kama mwanafunzi na Komredi Odoi ulikuwa mmoja wa wakufunzi watamu sana. Nakumbuka baadhi ya wachoraji komiki waliofaidi utaalamu wako kwenye kozi ile ni pamoja na Abdul Gugu, Robert Mwampembwa, Paul Ndunguru, Kati Kabatembo, Jiko Man, Willy Lyamba, Michael Sagikwa, Kato, David Chikoko, Fransis Bonda na wengineo.

Mbali na wewe Komredi Odoi, pia kulikuwa na wakufunzi wengine kama nguli la komiki, Tarmo Koivisto na Leif Packalen wote toka Finland. Ilikuwa kozi ngumu lakini kutokana na vituko vyenu walimu wetu hasa wewe Komredi Odoi, ikawa raha tu. Kila siku iendayo kwa Mungu ulihakikisha unatoka na mpya angalau moja ya kutuvunja mbavu.

Nakumbuka Komredi Odoi ulikuwa unashea rumu na mtani wangu wa Kisukuma, Bro James Gayo alimaarufu Kingo. Kuna siku msukuma alijitwika godoro lake zimazima, mchana kweupeee, akapita nalo kwenye korido, akalihifadhi chumba kingine ili giza likiingia asipate taabu! Msomaji ukitaka kujua zaidi kuhusu hadithi ya godoro, mtafute Gayo atakupa mkasa mzima.

Haya, kuna siku mlinzi mmoja, babu hivi pape tulipokuwa tunafanyia warsha, alikuja kuleta malalamiko kwamba, masela tulikuwa tunachelewa sana kurudi kulala. Isitoshe wakati tunarudi tulikuwa tunaimba wimbo wa Dr Remmy, ule wa siku ya kufa wandungu kwaheri kwa sauti kubwa halafu kwa ung’eng’e! 

Sasa wakati mlinzi anatoa malalamiko yake, Komredi Odoi ukawa unashuka nae kimchoro. Alipomaliza kumwaga lawama, tayari uso wake ulikuwa ushauweka kwenye pepa zamaaaaaani!

Moja ya kazi za Komredi

‘Afande babu’ alipotupa mgongo tu, Komredi Odoi ukaanza kutuonesha ile karikacha uliyomchora. Wacha tuangushe kicheko. Tukaongeza siku kadhaa za kuishi kiulaini na darasa likaendelea kuwa tamu zaidi na zaidi.

Komredi Odoi, wewe ni mmoja ya wachoraji komiki wa ukweli ambao mmepata kutokea Afrika. Nimejifunza mengi sana kutokana na mafunzo na kazi zako kaka.

Nakumbuka 2011, nilipokutana nawe Kenya, uliniasa jambo moja zuri sana. Ulisema, pamoja na ujio wa vifaa vya kisasa vya kielektoniki vya kuchorea, nisiache uchoraji wa asili. Ukimaanisha uchoraji wa kutumia karatasi, penseli, rangi, kifutio nk. Uliniambia, uchoraji wa kutumia kompyuta ni rahisi na wa haraka lakini unachangia kupoteza ubunifu, staili, utamu na kasi ya mkono.

Uliniambia nikilowea sana kwenye kompyuta, kuna siku naweza kukwama pale itakapotokea mteja akitaka michoro iliyochorwa kwa mkono. Nilikubaliana na wewe kaka kwa sababu tayari nimeshaanza kuonja ‘mavuno-hasi’ ya kuchorea komputa kila wakati.

Inaendelea kesho