Saturday, March 03, 2012

YANGA KIKAANGONI CAIRO LEO

Michael Momburi, Cairo
 
MABINGWA wa Tanzania, Yanga wanaingia dimbani leo wakiwa na lengo la kuvunja mwiko wa kufungwa na timu za kaskazini watakapoivaa Zamalek kwenye Uwanja wa Chuo cha Jeshi majira ya saa 12 jioni sawa na saa moja usiku za Tanzania.

Yanga
Katika mechi hii ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga inahitaji sare ya mabao 2-2 kusonga mbele au ushindi wowote kutokana na matokeo ya bao 1-1 katika mechi ya kwanza mjini Dar es Salaam, lakini suluhu au sare ya bao 1-1 ni nzuri kwa Zamalek.

Pamoja na ndoto hiyo wachezaji wa Yanga wanapaswa kusahau hali ya hewa ya baridi ambapo leo inatarajiwa kufika nyuzi joto 13 -14 wakati mechi hiyo itakapokuwa ikichezwa.

Pamoja na hali hiyo kocha wa Yanga, Kostadin Papic leo atalazimika kuendelea kutumia mfumo wake wa 4-3-3 na kuhakisha anapata bao la mapema litakalomwezesha kukaa kwenye mazingira mazuri ya kufuzu.

Hakuna shaka safu ya ushambuliaji wa Yanga itaanza na washambuliaji Davies Mwape, Asamoah na Hamis Kiiza akitokea pembeni huku Jerryson Tegete akiwa benchi.

Kutokana na kelele za mashabiki na viongozi wa Yanga, kocha Papic aanaweza pia akampa Tegete kuthibitisha ubora wake mbele ya ngome ya Zamalek.

Safu ya kiungo itaongozwa na Haruna Niyonzima akipata ushirikiano mkubwa kutoka kwa Nurdin Bakari aliyekuwa majeruhi pamoja na Juma Seif 'Kijiko' katika kuhakikisha wanavuruga mipango yote ya Zamalek.

Niyonzima
Kurejea kwa Ahmed Hossam MidoĆ® aliyekuwa nje kwa miezi miwili na kiungo Mahmoud Abdul-Razek 'Shikabala' kwa Zamalek kutamlazimisha kocha Papic kutoa mbinu mpya kwa ngome yake.

Nahodha wa Yanga, Shadrack Nsajigwa na beki wa kushoto Stephan Mwasika bado hawaonyeshi kiwango cha kuvutia tangu waliporejea baada ya kuwa majeruhi kwa muda mrefu.

Mabeki wa kati Nadir Haroub na Athuman Idd watakuwa na jukumu moja kubwa la kuhakikisha mshambuliaji Razak Omotoyossi na Mido hawachezi mipira yote ya krosi kutoka kwa Shikabala.

Haki za matangazo ya mchezo huo zimenunuliwa na klabu ya Al Ahly mwezi mmoja uliopita uliopita.

BARIDI

Kocha Papic amesema wameanza kuzoea hali hiyo na hawana jinsi kwani inabidi kukabiliana nayo, ingawa usiku hali ya hewa hubadilika na kutesa zaidi.

Papic alisema hawana wasiwasi na wako tayari kwa lolote na kama itabidi wachezaji watavalishwa glovus ila hapendi suala la hali ya hewa likuzwe sana kiasi cha kuchanganya wachezaji ingawa amekiri ni tatizo ila hawana jinsi tena.

Wachezaji wamelalamika baridi huku baadhi yao akiwamo Kenneth Asamoah wakiomba watafutiwe glovus ili kuendana na hali ya hewa na baridi hususani leo saa 12 jioni watakapocheza. 
Asamoh

"Naomba nitafutie glovus zozote nyepesi utakapokuja nitakulipa," alisikika Asamoah akimnong'oneza Afisa mmoja wa ubalozi wa Tanzania mjini hapa anayeshughulika na Yanga.

Kocha msaidizi wa Yanga, Fred Minziro alisema,"Sisi tunaokaa pale kwenye benchi sijui itakuwaje hiyo baridi ni kali sana halafu usiku upepo unachapa sana kwenye miguu."

UWANJA
Uwanja wa Chuo cha Jeshi ulioko nje kidogo ya Jiji la Cairo una uwezo wa kuchukua mashabiki 22,000, lakini leo utakuwa mweupe  kutokana na CAF kuifungia Zamalek.

Watanzania wanaoishi mjini hapa wamedai huenda kukawa na idadi kubwa ya askari ambao watakuwa kama walinzi, lakini wakitoa msaada kwa wenyeji washinde.

Katika Uwanja huo wa jeshi inaelezwa kuwa mashabiki huwa hawapendi kwenda kutokana na ulinzi mkali mno wa wanajeshi ambao hauwaruhusu kupiga mafataki na makelele yao ndani ya mazingira hayo.
Nurdin

Wanachama mbalimbali wa Yanga waliosafiri hadi hapa wakiongozwa na mwanachama mashuhuri wa Yanga, Wampunga wamekuwa wakihaha kuhakikisha kambi inakuwa salama na wachezaji hawagusi kitu chochote bila idhini ya viongozi wao ingawa wamekuwa wakiwakataza kuzungumza na vyombo vya habari vya Misri.

Kikosi cha kwanza huenda kikawa hivi; Shaaban Kado, Shadrack Nsajigwa, Stephan Mwasika, Athumani Idd 'Chuji', Nadir Haroub, Juma Sefu 'Kijiko', Nurdin Bakari, Haruna Niyonzima, Kenneth Asamoah/Jerryson Tegete, Davies Mwape na Hamis Kiiza. [Kwa mujibu Gazeti la Mwananchi]