Sunday, March 04, 2012

MADAKTARI KUGOMA JUMATANO

Na Beatrice Shayo

-Wasema utakuwa mgomo wa kihistoria
-Washikilia madai yao hayajatekelezwa
-Wasisitiza Dk. Mponda, Nkya waondolewe

Madaktari wakiwa wameshikana mikono kuashiria mshikamano kwa kauli moja ya kuanza mgomo siku ya Jumatano ijayo wakati walipotoa tamko lao katika mkutano wa uliofanyika jijini Dar es Salaam jana.

Madaktari wametangaza kuanza mgomo mwingine Jumatano ijayo baada ya Serikali kushindwa kuwatekelezea mahitaji yao kama walivyokubaliana katika kikao chao kilichopita.
Kati ya mahitaji yao ni kuitaka Serikali kuwaondoa madarakani Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda na Naibu wake Dk. Lucy Nkya.

Katika kikao chao cha jana wameridhia kwa pamoja kuwa endapo Serikali haitachukua hatua dhidi ya suala hilo watafanya mgomo mkubwa wa aina yake kihistoria Jumatano (Machi 7) ili madai yao yaweze kutekelezeka.

Akitangaza tamko hilo jana jijini Dar es Salaam katika mkutano wao wakiwemo madaktari wa mikoani, Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari nchini (MAT), Dk. Godbless Charles, alisema kuwa suala hilo limeridhiwa na madaktari wote.

Baadhi ya madaktari waliohudhuria mkutano wa jana.
Alisema viongozi hao wamekuwa ni kikwazo katika utekelezaji wa madai yao na kwamba wamekuwa wakichangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa mgomo huo.

Alisema kwa sasa wanaipa muda Serikali kufanyia maamuzi suala hilo na endapo itakaa kimya hadi Jumatano ijayo, wataweka vifaa vyao chini na kugoma kufanyakazi mpaka hapo kitakapoeleweka.

Dk. Charles alisema kuwa juzi walikutana na kamati iliyoundwa kwa ajili ya kuchunguza madai yao kwa ajili ya majadiliano ya utekelezaji wake.

Alisema walivyokutana na kamati hiyo walijua wanajadili moja kwa moja kuhusiana na madai yao ambapo waliwaambia kwamba mpaka kufikia hatua ya makubaliano ni lazima masuala matatu muhimu yafuatwe.
Waliyataja masuala hayo kuwa ni kuandaa mazingira ya utekelezaji wa hayo watakayoafikiana, kujadili madai ya madaktari pamoja na kutiliana sahihi makubaliano hayo.

Hata hivyo, Dk Charles alisema utekelezaji wa suala la pili na la tatu unakwenda sambamba na suala la kwanza ambapo linataka kuondolewa kwa viongozi hao wawili ndipo utekelezaji wa mengine ufuatwe.

Alisema madaktari hawana imani na viongozi hao kwa kuwa hawataweza kujadili mambo ya chini kwa kuwa ya juu hayajatekelezwa.

Madaktari hao walidai kuwa awali walipendekeza viongozi wa wizara hiyo kuwajibishwa lakini matokeo yake Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliwawajibisha, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Deo Mtasiwa, huku wahusika wengine wakiachwa.

Aidha, walisema Pinda aliwajulisha kuwa yeye hawezi kumwajibisha Dk. Mponda na Dk. Nkya kwa kuwa wameteuliwa na Rais.

Madaktari hao walisema kuwa mpaka sasa hawajajulishwa ni hatua gani zitachukuliwa dhidi ya viongozi hao ambao wamedai kuwa wamechangia kwa kiasi kikubwa kutokea kwa vifo vya wagonjwa.

Walisema kuwa wameshangazwa na kauli ya Dk. Mponda kueleza kuwa mpaka ajisikie kujiuzulu ndipo atafanya hivyo wakati yeye na wenzake wamesababisha madhara hayo kutokea.

Aidha, walisema pamoja na Rais Kikwete kutangaza kumaliza tatizo lao na kusisitiza kutokuwepo kwa mgomo huo bado wanapinga vikali jambo hilo na kueleza kuwa mgomo huo utakaoanza utakuwa ni mkubwa na wa kihistoria nchini.

 "Tuliambiwa Rais hayupo, tunashindwa kuelewa mpaka sasa bado hajarudi na je ni hatua gani inachukuliwa hatuwezi kwenda mbele kujadili kabla hilo halijatekelezwa," alisema.
Aidha Dk. Charles alisema kuwa Serikali imeona kuwa madai yao makubwa ni nyongeza ya mshahara bila kuwaboreshea mazingira ya kazi kwani wanafanya kazi katika mazingira magumu.

"Hivyo vijisenti vyao hata wakituongezea tunaweza kuvikataa sasa watatuongezeaje fedha bila kutuboreshea mazingira ya kazi mgonjwa anakuja hakuna vifaa matokeo yake anafariki tumechoka kuona wagonjwa wakitufia kwa kukosa dawa ifike wakati taaluma yetu iheshimike kwani sisi sio wanasiasa," alisema.

Kwa upande wake mjumbe wa kamati ya madaktari, Dk Steven Ulimboka, alisema kuwa lengo la mgomo huo ni kuishinikiza Serikali kuwapatia madai yao ya msingi ambayo waliahidiwa kufanyiwa kazi.

Alisema hiyo siku ya mgomo hawana haja ya kuendelea kufanya mkutano kila mmoja atatakiwa kufanya mambo yake mengine baada ya vifaa vyao kuwekwa chini. Alisema kwa sasa wanakwenda hatua kwa hatua na mgomo wa sasa utakuwa mkubwa kuliko wa awali mpaka hapo madai yao yatakapotekelezwa.

Alisema umma unatakiwa kuelewa kuwa Serikali ndio inawasababishia madhara kuwepo pale wanapofanya mgomo na kwamba taaluma yao imekuwa ikidharauliwa badala ya kuheshimika.
Alisema wameshindwa kuelewa ni kwanini kamati hiyo imewacheleweshea kuwapatia majibu licha ya kwamba waliwaongezea muda wa wiki mbili ili waletewe taarifa kuhusiana na utekelezaji wa madai yao kama walivyoagizwa na Waziri Mkuu.

Wakati wakiwa kwenye kikao hicho, mmoja wa madkatari hao, alimtaka Rais wa MAT, Dk. Namala Mkopi , kuwasiliana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia, kuwajulisha kama kuna hatua zozote zilifikiwa kuhusu suala lao la kuondolewa kwa viongozi hao ili waweze kuendelea kujadili masuala mengine muhimu.

Hata hivyo, Dk. Mkopi alisema alifanikiwa kuongea na Ghasia na kumjibu kuwa hafahamu lolote kuhusiana na suala la viongozi hao na kwamba kuwajibishwa kwao kuko nje ya uwezo wake. Aliongeza kuwa Ghasia alimwambia kwa wakati huo (jana) alikuwa ameanza likizo.

Hivi karibuni madaktari walifanya mgomo kwa nia ya kuishinikiza Serikali iwapatie madai yao ikiwemo nyongeza ya posho, posho ya mazingira hatarishi, posho ya muda wa ziada pindi wanapokuwa kazini, kupatiwa nyumba, usafiri pamoja na kadi ya bima.
Madaktari hao waliwasilisha madai nane kwa Pinda ambapo aliahidi kuyashughulikia katika kikao chao kilichopita na kuwajulisha kuwa ameunda kamati ya watu tisa kwa ajili ya kushughulikia madai yao. [Chanzo: Nipashe Jumapili]