ULE usemi
unaosema, ‘makocha wanaajiriwa ili watimuliwe’, umedhihirika baada ya taarifa
kutoka Klabu ya Chelsea, kumwaga kocha wake, Andre Villas-Boas, kufuatia timu
hiyo kusuasua kwenye Ligi Kuu ya Uingereza.
![]() |
Andre - Kushney |
Toka msimu
huu uanze, The Blues, wamekuwa na mwendo wa kinyonga na kuna hatihati huwenda
wakakosa moja ya nafasi nne za juu toka timu hiyo iliponunuliwa na Bilionea Roman
Abramovich.
Jana, Villas-Boas,
34, alishuhudia timu yake ikila kichapo kisichotegemewa cha 1-0 toka kwa West Brom, hali iliyopelekea Abramovich
kumchenjia Andre.
Kwa
mujibu wa taarifa inayopatikana kwenye tovuti ya Chelsea, jana, inasema: ‘Andres
Villa-Boas hatunae tena hapa Chelsea Football Club.
‘Bodi ya
timu inamshukuru kwa mchango wake kwa klabu na inasikitika kwamba inavunja
mkataba kabla haujakwisha’, ilisema taarifa hiyo.
‘Bahati
mbaya matokeo na uwezo wa timu unalegalega na hakuna dalili za kuboreka kwa
kipindi hiki’, iliongeza.
‘Chelsea
bado inapigana kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la FA pia inahaha kusaka
moja ya nafasi nne za juu kwenye ligi ya Uingereza, na lengo letu ni
kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye mashindano yote’, ilisema.
![]() |
Di Matteo - Ala kukuz |
‘Ili
kuhakikisha tunarudi kwenye mstari tumeona ni bora kufanya mabadiliko ya
mwalimu’, ilisema.
Nyota wa
zamani wa timu hiyo, Muitaliano, Roberto Di Matteo, amepewa kiti cha kuinoa
timu hiyo mpaka mwisho wa msimu huu’.
Di Matteo
ataanza kibarua Jumanne hii, wakati Chelsea itakaposhuka dimbani kuumana na wenyeji
Birmingham, kwenye mzunguko wa tano wa Kombe la FA.
Di Matteo
pia ana kimbembe kingine baadae mwezi huu cha kuhakikisha Chelsea, inatumia
uwanja wake wa nyumbani vizuri ili kuishinda Napoli, katika mchezo wa marudiano
wa Klabu Bingwa Ulaya. Mechi ya awali Chelsea ilichezea kichapo cha magoli 3-1.