Saturday, February 18, 2012

‘TEJA’ WHITNEY ELIZABETH HOUSTON APUMZISHWA LEO

-Familia yaita:  ‘si mazishi bali ni tukio la  ‘kwenda peponi’
-Mazishi ni kwa mwaliko maalum
-Aagwa na familia tu
-Bobby Brown chupuchupu kutoswa na familia

Baadhi ya watu maarufu wanategemea kuhudhiria mazishi ya Whitney Houston, leo(Jumamosi), kwenye kanisa lililokatika mji aliokulia na ambalo alipata kuimbia wakati wa utoto wake.

Mazishi hayo yatasindikizwa na nyimbo moroooooro toka kwa Aretha Franklin (mama wa ubatizo wa Whitney) na Stevie Wonder wakati ambapo Kevin Costner, mshiriki mwenzake kwenye muvi ya The Bodyguard, atasoma  wasifu wa marehemu. Alicia Keys and R. Kelly wanataraji kunogesha mazishi hayo pia.

Baadhi ya watu maarufu walioalikwa ni pamoja na Jay-Z na tunda lake, Beyonce, David Bowie, Mkongwe Elton John, Malkia Oprah Winfrey, Binamu wa Whitney, Dionne Warwick na muigizaji maarufu Bill Cosby.

Whitney, Brown na binti yao Kristina
Shughuli ya mazishi itaanza mchana kwa saa za kwa Obama kwenye kanisa la New Hope Baptist lilopo Newark, New Jersey, na  litarusha laivu kwenye luninga. Baadaye mwili wa marehemu Whitney, alifia hoteli ya Beverly Hilton , Los Angeles hivi karibuni, utapumzishwa kwenye makaburi ya Westfield yaliyo karibu na kanisa hilo.

Whitney atazikwa karibu na alipolala baba yake John, ambaye enzi ya uhai wake alipenda kumwita mwanae huyo ‘Nippy’(mnyama anayefugwa nyumbani kwa ajili ya kuburudisha, kurandaranda sebuleni, kwenda nae bichi, mitaani, mabustanini sio ulinzi)

Kadi ya mwaliko yasomeka maneno: ‘Kwenda Peponi’

Kwa moyo wa dhati, familia ya Houston Family inakualika kwenye tukio la ‘Kwenda Peponi’ Bi. Whitney Elizabeth Houston", baadhi ya maneno yanayosomeka kwenye kadi ya mwaliko. Dhana ya ‘Kwenda Peponi’ ni maarufu kwa Wamarekani weusi, ni sherehe kuliko mazishi. Inatoa heshima kwa marehemu na kusheherekea safari yake ya kwenda peponi kwa Mungu.

Waalikwa. Jay-Z na mai waifu wake, Beyonce
 Mume wa zamani wa Whitney, Bobby Brown nae atahudhuria mazishi hayo ili kumsapoti binti yake, Bobbi Kristina. Habari zinasema, Bobby alipewa mwaliko dakika za lala salama.
Nyota huyo wa R&B amekuwa amekuwa akinyooshewa kidole na familia ya Whitney kuwa ndiye aliyetia marehemu kwenye matumizi ya ‘unga’ na kuna nyakati walimtaka asimfuatefuate mtoto wao. Ndoa ya Bobby na Whitney iliyokuwa na misukosuko ilidumu kwa miaka 15. Mara tu baada ya mazishi, Mchizi, Brown atakula pipa maalumu kuwahi tamasha la bendi yake.

Jana mtoto wa marehemu, Bobby Kristina aliungana na familia yake kwenye tukio la siri la kuaga mwili wa mama yake aliyefariki akiwa na umri wa miaka 48. [Chanzo: Mashirika]