Friday, February 24, 2012

MAUAJI YA RAIA SONGEA: JESHI LA POLISI LASHIKILIA POLISI WANNE

JESHI la Polisi Mkoani Ruvuma, linawashikilia askari wake wanne kwa tuhuma za mauaji ya raia kwa kutumia risasi za moto katika purukushani zilizotokea juzi Mjini Songea. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Michael Kamhanda, alisema jana kuwa askari hao wametiwa nguvuni na wanaendelea kuhojiwa ili kujua kama kulikuwa na uzembe katika utekelezaji wa kazi yao.

Chini ya ulinzi
Kamanda huyo alisema, askari hao watahojiwa baada ya kuundwa kwa tume ya kuchunguza sokomoko hilo, na tume hiyo ikibaini kuwa kulikuwa na uzembe, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ikiwamo kufikishwa mahakamani.

Hata hivyo kamanda Kamhanda hakutaka kutaja majina wala vyeo vya watuhumiwa hao kwa maelezo kwamba ni mapema mno, pia sababu za kiusalama.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema ametuma kikosi cha maofisa waandamizi  kutoka  makao makuu ya jeshi hilo, kikiongozwa na Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo, Kamishna Paul Chagonja kwenda mjini Songea kufanya uchunguzi wa ghasia hizo.

Juzi waendesha bodaboda kwa kushirikiana na wananchi waliandamana kuelekea kituo cha polisi wakipinga mauaji ambayo yanahusishwa na unyofolewaji wa viungo.