Thursday, March 01, 2012

MATAIFA YA AFRIKA: CAMEROON YASHINDA KWA MBINDE, NIGERIA YATOKEA MBAVUNI, UGANDA YACHEZEA KICHAPO

JANA kulifanyika michezo kadhaa ya kutafuta tiketi za kufuzu kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika, 2013, nchini Afrika Kusini. 

Ikicheza nyumbani, Rwanda, iliibana mbavu barabara, Nigeria na kwenda suluhu. Wakati Nigeria wakichekelea sare, vigogo wengine wa soka wa Afrika, Cameroon, wao walianza mbio za kwenda Afrika Kusini, kwa ushindi wa manati wa goli moja kavu dhidi ya Guinea-Bissau waliokuwa wakicheza kwao.

Wakiwa bado na jinamizi la kukosa fainali za Mataifa ya Afrika zilizopita, vigogo hivyo, vilijipanga kuhakikisha vinaanza kuweka mazingira safi mapema. Wakicheza mechi yao ya kwanza ya mashindano chini ya kocha mzawa, Stephen Keshi, Nigeria, waliponea chupuchupu kudadavuliwa na wenyeji, Rwanda ambao walionekana kuwazidi maarifa kwa kuelekeza mashambulizi ya nguvu kwenye imaya ya wageni walionekana kushindwa kumudu mziki wa vijana wa Kagame.

Eric Maxim Choupo-Moting - Mfungaji wa bao pekee
Wakati Nigeria wakitaabika, wenzao Cameroon, wakiwa bila nyota wao waliyemsimamishwa, Samuel Eto'o, walipata ushindi mwembamba dhidi ya Guinea Bissau, kupitia kwa straika, Eric Maxim Choupo-Moting dakika tatu kabla mpira kwisha.

Kwingineko, Cape Verde na DR Congo wakazimung’unya kiulaiini Madagascar na Seychelles kila mmoja. Ikicheza na wachezaji 10, Cape Verde imeshinda 4-0 mjini Antananarivo, kwa magoli ya Ryan Mendes, Dady, Fernando Varela na Tony.

Chui wa Kabila, DR Congo, nao wakaikandamiza bila huruma Seychelles kwa magoli 4-0. Alain Kaluyituka alianza kucheka na nyavu kabla ya Tresor Mputu na Jeremie Basilwa kupigilia misumali ya iliyofuatia.

Pamoja na Burundi kuifurusha Zimbabwe kwa magoli 2-1, ushindi hupo umeingia doa baada ya Kocha wa timu hiyo Adel Amrouche, kutangaza kubwaga manyanga kufuatia maandalizi mabaya ya kikosi hiko. ‘Naachia ngazi, siwezi kuendelea kufundisha timu isiyoandaliwa ipasavyo kimashindano’, alisema Mbeljiani huyo mara tu baada ya mechi.

Mavugo Lody alikuwa wa kwanza kucheka na nyavu za wageni dakika chache baada ya kuanza kipindi cha pili. Musona anayekipiga Ujerumani, aliisawazishia Zimbabwe na kuonekana kama mechi ingekwisha kwa sare, lakini Valery Nahayo alizima ndoto za wageni kwa kupachika bao la ushindi dakika mbili kabla ya kipenga cha mwisho.

Kutoka Nairobi, pamoja na kukosekana kwa nyota wao, McDonald Mariga, majirani zetu, Kenya, wamefanya kile kitu roho inapenda kwa kuinyuka Togo bakora 2-1. James Situma, aliifungia goli la kwanza Kenya kwa kichwa kufuatia mpira wa kona lakini Razak Boukari akaisawazishia Togo, ambao walikuwa wakicheza mechi yao ya kwanza chini ya kocha, Didier Six.


Kipindi cha pili, Allan Wanga, akatupia mpira wavuni na kuipa ushindi Kenya ambayo sasa ina kibarua kizito cha kulinda ushindi huo kwenye mchezo wa marudiano, Mjini Lome.

Wakicheza nyumbani, Chad, wameifunga Malawi 3-2 wakati ambapo Uganda wamechezea kichapo cha magoli 3-1 toka kwa Congo waliokuwa wakicheza nyumabi.

Matokeo kamili ya mechi za jana; Madagascar 0-4 Cape Verde,Tanzania 1-1 Mozambique, Rwanda 0-0 Nigeria, Ethiopia 0-0 Benin, Burundi 2-1 Zimbabwe, Kenya 2-1 Togo, Chad 3-2 Malawi, Seychelles 0-4 DR Congo, Congo Brazzaville 3-1 Uganda, Liberia 1-0 Namibia, The Gambia 1-2 Algeria, Guinea Bissau 0-1 Cameroon na Sao Tome 2-1 Sierra Leone. [Chanzo: Mashirika]