Saturday, February 25, 2012

MAMA PINDA: VYAMA HAI VYA MICHEZO VIPEWE RUZUKU

MKE wa Warizi Mkuu, Mama Tunu Pinda, ameiomba serikali kutoa ruzuku kwa vyama hai vya michezo vinavyojitahidi kuendeleza michezo nchini. Mama Pinda meyasema hayo wakati alipokuwa akifungua mashindano ya netiboli kwenye Viwanja vya Chang’ombe, Jijini Dar es Salaam leo.

Akitoa mfano, Mama Pinda alisema, bajeti ya timu ya Taifa ya netiboli iliyo kambini Kibaha, kujiandaa na Kombe la Netiboli la Afrika la netiboli ni Tsh. 43,250,000, ambazo ni kwa jili ya malazi, chakula, vifaa na posho za wachezaji.

Mama Pinda: 'Wadau, ipigeni tafu Taifa Queens itupe raha'
Alisema laiti gharama hiyo ingegawanywa kwa wanawake wote wapenda michezo nchini, kila mmoja angechangia fedha kidogo sana. Ili timu ya netiboli ya taifa ifanye vizuri, michango ni lazima.

Alisema kuna wafadhili wengi, tatizo wamejikita sehemu moja pengine ni kwa sababu hawajahamasishwa kuchangia netiboli. Amewahimiza wapenda michezo, wajitokeze kuonesha uzalendo kwa kuichangia Taifa Queens.

Tayari timu za Bandari, Temeke Queens, Kambangwa na Tumaini(za Dar es Salaam), Black Sister(Pwani), Ras Lindi(Lindi), Kurugenzi Tandahimba  na Umoja Queens ya Ndanda zimesharipoti. Katika mchezo wa ufunguzi leo, Bandari imeichapa Temeke Queens kwa magoli 38-24.

Ligi hiyo itaendelea kesho jioni, ambapo Tumaini itacheza na Black Sister, ikifuatiwa na mchezo kati ya Ras Lindi dhidi ya  Kurugenzi Tandahimba. Umoja Queens na Kambangwa watamalizia.