Thursday, February 16, 2012

KUMBE CHIPOLOPOLO UTAALAMU SI UWANJANI TU NA KWENYE UGIMBI PIA

RAIS wa Chama cha Mashabiki cha Zambia, Bw. Yotam Mwanza, amewashauri wachezaji wa wa Timu ya Taifa ya Zambia, Chipolopolo – ambao wanasifika kwa kukata maji, kutonywea pombe fedha walizozawadiwa na serikali  baada ya kutwaa kombe hivi karibuni. Serikali ya nchi hiyo imetoa kitita cha dola 59,000 kwa kila mchezaji.

Akiongea na The Independent Post  muda mfupi baada ya Rais, Michael Sata kuweka ua sehemu ya kumbukumbu ya wachezaji wa Chipolopolo walioteketea kwenye ajali ya ndege mwaka1993, nchini  Gabon, Mwanza aliwataka wachezaji kutumia ‘mahela’  hayo kwa uangalifu.

Chipolopolo - full shangwe
Nafikiri wachezaji wanahitaji kujilinda wenyewe. Wasijisahau. Wasije wakapigia ulabu fedha zote’,  alisema Mwanza.

Wakati mashindano yakiendelea,  Zambia ilimtimua winga wake hatari anayekipiga sauzi kwa Mzee Madiba, Clifford Mulenga kwa sababu alikuwa hashikiki kwa maji ya mende.

Historia inaonesha kuwa, Wanachipolopolo si nyota tu viwanjani bali pia ni hodari kwenye ugimbi. Taarifa zinasema, wakati wa fainali za Afrika, viongozi walichoka, hata walipowakuta wako bwii, waliwasamehe. Baadhi yao walitoroka kambini  na kutokomoa kona kula ‘mayi’. Inadaiwa pia kwa ‘vicheche’ walikuwa hawajambo pia.

Akiongea kupitia Radio ya Taifa ya Zambia, Waziri wa Michezo, Chishimba Kambwili,  amesema, selikali itamzawadia kila shujaa dola 59,000 ambazo ni mbali na watakazovuta toka kwa taasisi nyingine.

Mulenga - bila 'mayi' silali
Ikicheza huku ikiwa na kumbukumbu ya vifo vya kaka zao vilivyotokana na ajali ya ndege iliyotokea Bahari ya Atlantic, pwani ya Gabon, Wanachipolopolo waliwatoa kamasi Ivory Coast kwa penati 8-7 baada ya kwenda suluhu kwa 120 katika mchezo wa kuvutia wa fainali uliopigwa Libreville, Gabon, Jumapili  iliyopita.

Katika ajali ile, abiria wote 30 wakiwepo Wanachipolopolo waliokuwa kwenye dege la jeshi safarini kwenda Dakar, Senegal kwa mechi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mwaka 1994  nchini Marekani dhidi ya Simba wa Teranga, walikufa.

Wachezaji waliofariki ni Efford Chabala, Richard Mwanza, John Soko, Whiteson Changwe, Robert Watiyakeni, Samuel Chomba, Winter Mumba, Godfrey Kangwa, Kenan Simambe, Eston Mulenga, Derby Makinka, Moses Chikwalakwala, Wisdom Mumba Chansa na Numba Mwila.


Wengine ni Kelvin "Malaza" Mutale, Timothy Mwitwa, Moses Masuwa na 

Patrick "Bomber" Banda.
Chanzo: Mashirika