Monday, February 20, 2012

'KICHWA NGUMU' BOBBY BROWN AONJESHWA SHUBIRI MSIBA WA ‘MKEWE’ WHITNEY HOUSTON

-Familia ya Whitney Houston yakana Bobby Brown kutimuliwa
-Wapambe wa Brown watimuliwa sehemu ya familia
-Brown adai watu wa usalama wamemfanyia sivyo ndivyo

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Mwanamuziki Bobby Brown, Jumamosi iliyopita, alitia pua kwa muda mchache kwenye misa ya mazishi ya aliyekuwa mkewe Whitney Houston kisha akala kona na kuwaacha waombolezaji waliohudhuria tukio hilo midomo wazi.

Brown aliyekuwa ameambata na ‘usingizi’ wake wa sasa, Bi. Alicia Etheridge, amewatupia lawama watu wa usalama kwa kutoitendea haki familia yake na kudai alitiliwa kiwingu asiwe karibu na mwanae kauli ambayo imepigwa vikali na familia ya marehemu.

 Bobby(kushoto) na mai waifu wake
Brown aliyeambatana na wapambe kibao, aliingia kanisani na kukaa mbele sehemu maalumu iluyotengwa kwa ajili ya familia ya marehemu kabla ya kuambiwa anyanyuke na kukaa mahala pengine. Brown aliingia kanisa la New Hope Baptist kama muombolezaji wa kawaida na alikuwa mbali na familia ya Houston. Alionekana mwenye huzuni, macho mekundu na alikuwa akigeuzageuza shingo huku na kule.

Akalikaribia jeneza la ‘mkewe’, kisha akalipita na kwenda nyuma ya kanisa. Ghafla akala kona.

‘Mimi na binti yangu tulialikwa kwenye misa ya mke wangu wa zamani, Whitney Houston’, ilisema taarifa iliyotolewa baadae.

‘Tulikuwa tumekaa karibu na watu wasalama. Wakatuhamishia sehemu tatu tofauti. Nashindwa kuelewa kwa nini jamaa waiyanyase familia yangu hivi, mbona waombolezaji wengine hawakuguswa kabisa. Baadae watu wa usalama wakanizuia kabisa nisimtie machoni binti yangu, Bobbi Kristina’ ilisema taarifa hiyo.

‘Ili kuepusha kiwingu, niliamua kulimwagia busu jeneza la waifu wangu wa zamani na kutambaa…Nitaendelea kumuenzi Whitney kwa heshima zote. Taarifa hiyo imeongeza.

Bobby jukwaani usiku huohuo
Kutokana na utaratibu ulivyokuwa umepangwa, Brown alitakiwa kuambatana na watu wawili badala yake akaja na kikosi cha 10, mtu wa karibu na familia ya Houston aliviambia vyombo vya habari huku akiomba jina lake lihifadhiwe kutokana na unyeti wa msiba wenyewe.

Familia ilimtaka Bobby aendelee kukaa sehemu iliyotengwa kwa ajili ya familia isipokuwa kundi lake likajichanganye na waombolezaji wa kawaida ili kutoa nafasi kwa mama wa Whitney, Bi. Cissy na wanafamilia wengine. Bobby akajibu, ‘hiyo itakuwa ngumu’. Mtoa taarifa huyo amesema.

Baada ya Brown kujifanya mbogo, familia ikaomba msaada wa manjagu.
Polisi wakarudia kile kilichosemwa na familia kabla, Bobby akasema, haiwezekani, kisha akatimua na wapambe wake. Ila ukweli unabaki palepale kwamba, familia ilimwalika Bobby kwa roho nyeupe’, mtoa taarifa huyo aliongeza.

Ili kuonesha ukidume wake, Bobby alipanga kupagawisha wapenzi wake kwenye onesho la bendi yake ya New Edition baadae usiku, onesho lililochukuliwa kama sehemu ya kumliwaza Bobby kutokana na maswahibu yaliyompata, mpambe wa karibu wa Bobby alisema.

Nilikula kiapo cha ndoa - Whitney
Bobby na Whitney walifunga ndoa 1992 ambapo mwaka 2007 walimwagana. 1993 walimzaa Bobbi Kristina Brown, aliyelelewa muda mwingi na Whitney. Walipofunga ndoa Julai 1992, maswali mengi yalijitokeza, wengine waliamini ulikuwa wakati wa Bobby kujiosha kutokana na jamii kumchukulia kama ‘muhuni’ na kuna wakati alikiri kuwa na watoto watatu.

Whitney aliyapotezea madai hayo na kusema, yeyote anayeichimba ndoa yake basi haelewi kiapo cha ndoa alichokula kwenye ndoa yake. Mwishoni mwa 1990 na mwanzoni 2000 taarifa zikaanza kusambaa kuhusiana na mama huyo kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya, matatizo ya kiafya na songombingo za asha ngedere kwenye ndoa yake. Mauzo ya albamu yake aliyoitoa kipindi hiko hayakuwa mazuri na sauti yake ikaanza kuwa na mikwaruzo.

 
Akihojiwa na mtangazaji Diane Sawyer, ABC mwaka 2002, Whitney alikiri kutumia unga na akanukuliwa akisema ‘Adui mkubwa kwenye maisha yake ni nafsi yake. Mimi ni ama rafiki mzuri au adui’. [Chanzo: Mashirika]