Thursday, February 23, 2012

HATIMAE TEVEZ ANYWEA, AILAMBA MIGUU MANCHESTER CITY

Manchester City, England. 

Baada ya kuonesha bifu na kocha wake,  Roberto Mancini kwa takribani miezi mitano, hatimae mshambuliaji hatari, Carlos Tevez jana usiku, aliipigia goti na kuiomba radhi klabu yake ya Manchester City. 

Tevez aliongeza sumu kwenye bifu hilo kwa kususa kucheza hali iliyomsababishia kukatwa paundi milioni 10, zinazojumuisha mshahara, marupurupiu na faini.

Tevez: 'Mancini inatosha sasa bana'

‘Tevez ametubu na anajutia ‘wehu’ alioufanya katika siku za karibuni’, ilisema taarifa iliyotolewa na klabu yake. Tevez alirejea kundini Jumanne iliyopita baada ya kuichunia klabu yake na kuingia mitini kwa miezi mitatu bila ruhusa. Tevez amesema: ‘Naomba radhi toka moyoni kwa kila niliyemkosea kwa siku za karibuni. Sasa akili yangu ni kuitumikia klabu yangu ya Manchester City’.


Tevez pia amefuta malalamiko yake aliyokuwa akiilalamikia klabu yake ambayo yalikuwa yasikilizwe siku chache zijazo na Jopo la Ligi Kuu ya Uingereza. Ili kujiweka fit, tayari Tevez ameshanza mazoezi ya kufa mtu.

Tevez na washauri wake wameomba radhi baada ya kikao chao na Mratibu wa klabu hiyo, Brian Marwood kwenye uwanja wa mazoezi wa Man City jana.

Meneja Mancini hakutaka kushiriki kikao hiko kwa madai kuwa alikuwa bize akiandaa kikosi chake na gemu ya leo(Jumatano) dhidi ya Porto. [Chanzo: Mashirika]