Wednesday, May 04, 2016

MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA YA TUZO ZA UMAHIRI WA UANDISHI WA HABARI (EJAT) 2015

Utambulisho: Baadhi ya majaji wa Shindano la Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari (EJAT) 2015. Kutoka kushoto ni Bw. Jesse Kwayu, Bw. Nathan Mpangala, Bw. Juma Dihule, Bw. Kiondo Mshana, Bi. Pili Mtambalike na Dkt. Joyce Bazira Ntobi.
Mchora vibonzo bora wa EJAT 2015, Said Michael "Wakudata"  (kushoto), akinong'ona jambo na Abdul Kingo "Kaboka Mchizi" huku wakishushia vinywaji laini.
Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari (EJAT) 2015: Kutoka kulia, Said Michael "Wakudata" - mchoraji bora wa vibonzo wa EJAT 2015, Nathan Mpangala - Jaji EJAT 2015 na Abdul Kingo "Kaboka Mchizi" - Mshindi wa pili wakiwa wamekula pozi muda mfupi baada ya washindi kulamba vilambwaji vyao katika hafla iliyofanyika Ukumbi wa Mlimani City, Jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.

Tuesday, May 03, 2016

JAJI WA SHINDANO LA TUZO ZA EJAT 2015, NATHAN MPANGALA ALIPONGEZA BARAZA LA HABARI TANZANIA (MCT)

MMOJA wa majaji wa Shindano la Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari (EJAT) 2015, ambaye pia ni mchoraji vibonzo maarufu nchini, Nathan Mpangala amelipongeza Baraza la Habari Tanzania (MCT), kwa kumpa heshima ya kuwa mmoja wa majaji wa tuzo hizo zilizofanyika wiki iliyopita Jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia ushiriki wake katika shindano hilo, alisema toka kinyang'anyiro hiko kianze mwaka 2009 hakijawahi kuwa na jaji mchora vibonzo. Safari hii MCT wameliona hilo. Ni jambo zuri na la kupongezwa.

“Yanapofanyika mashindano ya aina yeyote yale, ni vema yakahusisha watu waliobobea katika eneo husika ili waweze kusaidia kutoa miongozo,” alisema Mpangala.

Jopo hilo la majaji liliongozwa na Bi. Valerie Msoka, wajumbe wengine ni  Bw. Ndimara Tegambwage, Dkt. Joyce Bazira Ntobi, Bw. Ali  Uki, Bw. Jesse  Kwayu, Bw. Kiondo Mshana,  Bw. Juma Dihule, Bw. Godfrey  Nago na  Bi. Pili Mtambalike.
Jaji wa Shindano la Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari (EJAT) 2015, Nathan Mpangala (kushoto) akimkabidhi tuzo Bw. Mansour Jumanne wa SAUT FM ya Mwanza katika hafla iliyofanyika Ukumbi wa Mlimani City, Jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.
Baadhi ya majaji wa Shindano la Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari (EJAT) 2015, wakifuatilia utoaji tuzo wa shindano hilo lililofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, Jijini Dar es Salaam wiki iliyopita. Kutoka kushoto ni Bw. Nathan Mpangala, Bw. Juma Dihule, Bw. Kiondo Mshana, Bi. Valerie Msoka (Mwenyekiti), Bw. Ndimara Tegambwage na Dkt. Joyce Bazira Ntobi.

Wednesday, April 13, 2016

BICHUKA ATEMBELEA OFISI YA KIJASTI LEO

Mwanamuziki mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Hassan Rehani Bichuka (kushoto) wakibadilishana mawili matatu na mchora vibonzo maarufu nchini, Nathan Mpangala aka Nanihii katika ofisi ya Nanihii iliyopo Nafasi Art Space, jijini Dar es Salaam, leo. Nguli huyo alisema yeye ni mfuatiliaji mkubwa wa kibonzo kinachorushwa ITV.

Wednesday, April 06, 2016

JE, UNAPENDA KURASIMISHA KAZI YAKO YA SANAA? TARATIBU HIZI HAPA...

BARAZA LA SANAA LA TAIFA (BASATA)
TARATIBU ZA KUPATA USAJILI NA KUTAMBULIWA

Utangulizi

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ni Shirika la umma lililoundwa kwa Sheria ya Bunge Na. 23 ya Mwaka 1984. Pamoja na kazi nyingine za Baraza zilizoanishwa katika Sheria hii, Baraza lina jukumu la kusajili na kutoa vibali kwa wale wote wanaojishughulisha na shughuli za Sanaa na Burudani Tanzania Bara. (“Ni kinyume cha Sheria kujishughulisha na shughuli za Sanaa na burudani bila ya kibali cha BASATA”). Aidha, Baraza lina mamlaka ya kufuta usajili, kusimamisha shughuli, kusitisha kwa muda au kutoa adhabu nyingine kwa yoyote anaekaidi Sheria hii.

Wanaotakiwa kusajiliwa na Baraza ni:

·       Wasanii binafsi (ikiwa ni pamoja na walio katika vikundi mbalimbali)
·       Vikundi vya wasanii
·       Vyama
·       Mitandao ya wasanii
·       Mashirikisho ya Wasanii
·       Taasisi
·       Kampuni
·       Studio za kurekodi muziki na
·       Kumbi za Sherehe na Burudani

Utaratibu wa kujisajili
a) Chukua fomu ya maombi ya usajili kwa Afisa Utamaduni wa Wilaya ulipo, Ofisi za BASATA, au katika tovuti ya Baraza (http://www.basata.go.tz/downloads.php ).   
Jaza fomu nakala 3 na uambatanishe na
·         Katiba nakala 3 (msanii binafsi aambatanishe wasifu wake si katiba)
·         Picha(passport size) nakala 3 za kila kiongozi wa kikundi/taasisi/kampuni n.k.
·         Nakala ya muhtasari wa kikao cha wanachama/wamiliki wa kujadili kusudio la kujisajili      na kuipitisha Katiba, pamoja na majina ya waliohudhuria na sahihi zao.
·         Nakala ya hati ya mlipa kodi (TIN)
b)  Pitisha maombi yako kwa Afisa Mtendaji wa Mtaa/Kijiji aidhinishe.
c)  Pitisha maombi yako kwa Afisa Utamaduni wa Wilaya aidhinishe.
d)  Wasilisha maombi yako BASATA.

Faida za kujisajili na kufanya kazi kwa kushirikiana na BASATA
·   Kuendesha shughuli kwa mujibu wa sheria za nchi.
·  Kuwa rasmi/kutambuliwa kwa shughuli ya msanii binafsi, kikundi, chama n.k hivyo kufanya kazi kihalali
·   Kupata ushauri wa kitaalamu kuhusiana na kazi za Sanaa
·  BASATA kama shahidi wa Jamhuri hutoa utambulisho wa msajiliwa mahali popote panapohitajika kwa mfano wakati wa kufungua akaunti, shahidi mahakamani n.k.
·   Kusaidia pale kazi itakapohitajika kuwekewa ulinzi kisheria, kwa mfano kumtambulisha msanii COSOTA ili kuthibitisha kama kazi imefanywa na msanii/ kikundi au chama kinachotambulika kisheria.
·   Kuwa karibu na wasanii na wadau wa sanaa kwa kutafuta na kusambaza taarifa za fursa zinazopatikana katika tasnia ya sanaa mfano: maonesho na matamasha ya nje ya nchi.
·    Kusaidia kutatua masuala yahusuyo haki za wasanii zinaporipotiwa na wasanii.

Ada ya kibali kwa mwaka (kuhuishwa kila mwaka)
·       Msanii binafsi Tsh 40,000
·       Kikundi Tsh 40,000
·       Chama Tsh 50,000
·       Mtandao Tsh 50,000
·       Taasisi Tsh 50,000
·       Kampuni Tsh 200,000
·       Studio Tsh 200,000
·       Kumbi 300,000 – 1,000,000 (kulingana na hadhi na sifa ya ukumbi)

Gharama za usajili: Makundi yote yatalipia ada ya usajili Tsh 30,000 na gharama ya fomu Tsh 5,000 (gharama hizi hulipwa mara moja tu)

NB: Kwa walioko mikoani unaweza kutuma maombi yako kupitia kwa Afisa Utamaduni wa Wilaya, kufika BASATA au kutuma moja kwa moja BASATA kwa njia ya Posta. Kwa maoni na maelezo zaidi wasiliana nasi kupitia:

Katibu Mtendaji,
S.L.P 4779, Dar es Salaam- Tanzania
Ilala Sharif Shamba,
Simu : Tel: 2863748/2860485
Faksi : 0255 - (022) - 286 0486

Barua pepe : basata06@yahoo.com